Monday, November 25

Mwili wa aliekuwa askari wa kikosi cha KVZ wapatikana pamoja na bunduki.

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Ahmed Makaran, akiwaonyesha waandishi wa habari kutoka Vyombo mbali mbali vya habari Kisiwani Pemba, bunduki iliyopatikana aina ya AK47 na magazine yake, bunduki ambayo ilitoweka pamoja na marehemu askari wa vikosi vya SMZ aliekua ameuwawa(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

MWANDISHI WETU, PEMBA.

 

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba limefanikiwa kuupata mwili wa aliekuwa askari wa kikosi cha KVZ Khalfan Junedi mwenye miaka 25 aliuwawa baada ya wiki tatu zilizopita huko eneo la Ngwachani Wilaya ya Mkoani.

Pamoja na mwili huo pia lilifanikiwa kuipata bunduki aina ya AK47 katika eneo la Ngwachani Novemba 12 majira ya saa 2:00 usiku ambayo magazine yake ikiwa na risasi 21.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani amesema  mwili huo ulipatika katika kijiji cha chonga kwenye bonde la Kisitu mbwa.

Alisema kuwa, Novemba 15 walifanikiwa kuupata mwili wa askari huyo baada ya kumkamata mtu mmoja anaejulikana kwa jina la Ussi Foum Machano mkaazi wa Ngwachani, ambae aliwapeleka kwenye eneo alilofukiwa.

“Novemba 12 tulimkamata Ussi,  maeneo ya Chake Chake ambae tulimuhoji na ndipo akatwambia mahala ilipo bunduki na baadae kwenda kutuonesha eneo alipowekwa marehemu huyo”, alisema Kamanda Makarani.

Alieleza kuwa, baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi, walibaini kuwa marehemu huo kabla ya kifo chake alikuwa na majeraha ya kupigwa huku akiwa amekatwa baadhi ya viungo vya mwili wake.

“Taratibu zote za kiuchunguzi kuhusiana na mwili zimefanywa baadae mwili umesafirishwa kwenda Unguja kwa ajili ya mazishi”, alisema.

Alisema kuwa, upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika na kusema kuwa wanaamini watawakamata watu wengine waliohusika na tukio hilo.

Alifahamisha kuwa, Oktoba 28 mwa huu askari huyo pamoja na wengine walikuwa kwenye doria za kawaida, ambapo askari huyo alipotea majira ya saa 2:00 usiku akiwa na bunduki AK47.

“Baada ya kupotea, Polisi, vyombo vya ulinzi na wananchi waliendelea kufuatilia taarifa hiyo, yuko wapi na ananafanya nini huko aliko, masuala yalikuwa mengi”, alisema.

Aidha Kamanda Makarani aliwataka wananchi wa Ngwachani kurudi katika maeneo yao ya kuishi, ili waendelee na shughuli zao za maisha, kwani amani na utulivu imerejea.

“Walokuwepo maporini warudi na waliokuwepo nje ya Pemba warudi, sisi kimsingi tunawatafuta watu ambao kwa namna moja ama nyengine wamehusika na mauwaji ya huyo askari na sio wananchi wa kawaida”, alifahamisha.

Nae Mkuu wa upelelezi Richard Tadei Mchomvu aliwanasihi wananchi waliokimbia kwa kuogopa msako warudi ili waendelee na shughuli zao kiuchumi sambamba na kuwataka wanafunzi warudi kuendelea na masomo.

“Wananchi wa kijiji cha Ngwachani ambao walipata taharuki na kukimbia kwa kuogopa msako ambao ulifanywa na vikosi, warudi katika maeneo yao, sisi tutaendelea kufanya upelelezi kisayansi zaidi”, alisema.

Aidha aliwataka wale ambao wanahisi wametajwa na huku wakijua kuwa hawahusiki na tukio hilo, wafikie kituo cha Polisi kujisalimisha mwenyewe huku akiwaomba wananchi kuzidisha ushirikiano kwa Jeshi la polisi ili kuweza kuwabaini wahalifu waliohusika na tukio hilo.