WEKUNDU wa Msimbazi Simba spots Club wamesema, kuwa kufungwa na watani wao wa jadi Yanga katika mchezo wao wa juzi ni sahihi kwani wangewafunga katika mechi ile ingekuwa ni aibu kubwa kwao.
Hayo yalielezwa na Msemaje wa timu hiyo Haji Sande Manara, wakati alipokuwa akizungumza na wapenzi wa michezo Kisiwani Pemba, kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Suluhu yaliyoandaliwa na mbunge wa Jimbo la Gando Salum Mussa Omar, yaliyofanyika katika kiwanja cha Kinyasini Wete.
Manara alieleza kuwa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa msimu huu wameshachukuwa lililobaki ni kuwataka wapenzi wa Simba kusubiri taarifa ya timu yao huko Kigoma na ndio hapo itakapoeleweka kuwa Simba inafanana na nani.
“Mchezo wetu wa juzi ilikuwa ni lazima tuwaachie kwa sababu tungewafunga juzi ingekuwa ni aibu kubwa sana kwao, sisi ubingwa tumeshachukuwa sasa subirini taarifa zetu za huko Kigoma ndio mtakapojua kuwa Simba ni nani,”alisema Manara.
Mapema Manara alimpongeza mbunge wa Jimbo la Gando Salum Mussa Omar kwa kuandaa mashindano makubwa ambapo alieleza kuwa hajawahi kushuhudia mashindano kama hayo katika majimbo yote ya Tanzania.
“Na hii sasa itawafanya waheshimiwa wabunge wengine hususan ndugu yangu Khamis Mwinjaku (Mwana FA) kufanya jambo kama hili katika jimbo lake na ikiwezekana umzidi Salim,”alisema Manara.
Sambamba na hayo msemaji huyo wa wekundu wa Msimbazi alieleza kuwa michezo lazima ifanyiwe kipaoumbele kila hali kama zilivyo sekta nyengine zilizopo nchini.
” Ndugu yangu Salim hii umewekeza, hujaekeza kwa ajili ya leo umewekeza kwa mwaka 2025, sura za wananchi hawa zimasema kuwa upo tena,”alisema Manara.
Hata hivyo Haji Manara aliwapongeza sana wananchi na wapenzi wa soka Kisiwani Pemba kwa kujitokeza kwa wingi katika fainali hiyo na kuwataka kushirikiana na viongozi wao kwa kila hali.
Mapema Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alieleza kuwa mkoa wake unasisitiza na kuhimiza amani, umoja na mshikamano ambapo ndio utaoleta matunda mazuri katika mkoa huo.
“Tuchezeni mpira kwa salama na amani na kuondokana na mifakano isiyokuwa ya lazima, niwaombe sana wachezaji chezeni mpira kwa uaminifu, uadilifu na kuondokana na mchezo mchafu ambao utaweza kupelekea mmoja wetu kuumia au kupata kilema cha maisha,”alisema Salama.
Hata hivyo Salama aliwataka wasimamizi wa mchezo huo kuendesha kwa taratibu zote bila ya kupendelea upande wowote ule.
Nae Mbunge wa jimbo la Muhenza Khamis Mwinjaku (Mwana FA) alieleza kuwa jambo ambalo amelifanya mbunge wa Jimbo la Gando ni la mfano na ni la kuigwa.
“Jambo ambalo amelifanya mbunge mwenzangu ni zuri na linahitaji kuigwa,” alisema Mwana FA.
Katika mtanage huo timu ya Gando B iliweza kutoka kidedea kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Kizimbani na kujinyakulia kitita cha Tsh, milioni 7 na Kombe huku Kizimbani ikinyakulia Tsh, milioni 4 ikiwa ni mshindi wa pili.