NA ABDI SULEIMAN.
WANANCHI wa shehia ya Ole Wilaya ya Chake Chake, wamewashauri wazazi wenzao kuwa tayari katika suala zima la malezi ya pamoja ya watoto wao, pamoja na kutokuvivumilia na kuvifumbia macho vitendo vionvu vinavyotokea katika maeneo yao.
Wamesema kumekuwa na wimbi kubwa la vijana kuwashirikisha katika masuala ya wizi au ununuzi wa vilevi na baadae kuwapelekea jambo ambalo linahatarisha maisha ya watoto hao.
“Hivi karibuni mtoto mdogo alipewa bata katika kipolo apelike sehemu, bahati nzuri sisi tulishutka na kumuuliza aliyempa bata hao nani, alipotutajia tulijikusanya na kufuatilia wanakopelekwa ndipo tulipomtia hatiani muhusika wa tukio”alisema mmoja ya wanaharakati.
Fatma Abdalla Issa alisema wahalifu wanawatumia watoto katika masuala ya ulevi, ikiwemo kuwatuma kwenda kununua sigara jambo ambalo linaweza kuwaingiza hata watoto katika uvutaji wa sigara.
Rashid Suleiman alisema hali ya ulevi katika jamii ipo kwa asilimia kubwa, hivyo wataendelea kuzungumza na vijanao ili kuondoa masuala ya ulevi kwenye shehia yao.
Kwa upande wake Hamad Said Hamad alifahamisha kwamba dawa za kulevya zinauzwa katika maduka ya dawa za kawaida, jambo ambalo limekua likiwakera sana katika maeneo yao kwani watoto wadogo ndio wanaotumwa kununua dawa hizo.
Afisa sheria kutoka tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za kulevya Pemba Daudi Juma Suleiman, alisema kuna baadhi ya vijana wanapokosa Heroini wanakimbilia spitali au vituo vya afya kwenda kununua dawa tiba na kutumia ilia pate hisia.
Alifahamisha katika wiki ya maadhimisho ya kuelekea siku ya kupiga vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya duniani, zaidi ya shehia 10 wameweza kuzufikia na kutoa elimu na kuweka mikakati ya kupiga vita utumiaji wa dawa hizo.
“Wapo watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu baada ya kutumia dawa za kulevya, wananchi vizuri sasa kutoa taarifa na kuwa makini katika suala hili”alisema.
Hata hivyo aliwataka wazazi kuwa makini na vijana wao, katika suala la utumiaji, usambazaji, uuzaji wa dawa za kulevya ni tataizo kubwa na shehia yake ni kali sana kwa muhusika wa dawa hizo.
Afisa afya kutoka tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya Pemba, Dkt.Ali Yussuf Ali alisema dawa za kulevya ni janga la taifa na jamii pia inaathirika, hivyo kila mtu anapaswa kulikemea kwa nguvu zote.
Aliwataka viongozi wa dini, walimu wa madrasa na skuli kuhakikisha wanatumia nafasi zao kuwelimisha wananchi juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa jamii.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mkurugenzi Uchunguzi na udhibiti Juma A Zidikheri, kupitia ripoti ya kitengo cha poli cha kupambana na dawa za kulevya kipindi cha miaka tisa iliyopita, 2012 hadi 2020 jumla ya watuhumiwa 3,819 wakiwemo wanaume 3,577 na wanawake 233 wamekamatwa nchini wakijihusisha na dawa za kulevya.
Katika kipindi hicho jumla ya kilo 51.5 za heroini, kilo 2,946 za bangi, kilo 5.4 za valium na kilo 19.71 za kokeni zilikamatwa, huku ujumbe wa mwaka huu ni “Sema ukweli juu ya athari za dawa za kulevya okoa maisha”.