Dunia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi ya kuvutia, ambayo hukusanya watu wa mataifa mbalimbali kuyatembelea. Kawaida vivutio vingi vinawekewa utaratibu ukiwemo wa utunzaji na malipo.
Mwaka 2019, sekta ya utalii duniani ilichangia asilimia 10.4% ya pato ghafi la dunia. Lakini yapo maeneo mazuri yangeweza kuchangia zaidi, ila ni marufuku kukanyaga.
Mamilioni ya watalii hutembelea hifadhi za wanyamapori, milima mirefu, majumba ya kale, maeneo ya utamaduni na maeneo mengine yanayowavutia.
Lakini yapo maeneo duniani ambayo watalii wangetamani kutembelea lakini kwa sababu ya sifa zake na historia yake yanaleta kikwazo. Mengi yamekuwepo bila kutunzwa kitalii lakini yanavutia kwa historia yake na vilivyomo.
Mengine ni wanasayansi tu huruhusiwa kuyafikia kwa masharti maalumu, maeneo mengine wala hukatazwi kuyatembelea lakini yanahitaji moyo wa kipekee kuyatembelea.
Kwa wenye imani, wengine wanasema kuwepo kwa maeneo ya aina hiyo kunaonesha ukuu wa uumbaji wa Mungu.
Ingawa yapo maeneo zaidi ya 30 yenye sifa hizi, lakini BBC inakuletea orodha ya maeneo sita ambayo watalii mwiko kuyatembelea licha ya uzuri na historia ya kuvutia ya maeneo hayo.
1. Mapango ya Lascaux, Ufaransa
Haya ni mapango marefu yanayopatikana kaskazini mashariki mwa Ufaransa. Ni moja ya mapango ambayo kunapatikana michoro mizuri na maarufu zaidi ya kihistoria duniani. Inaelezwa ni michoro ya siku nyingi ya enzi za mababu wa mababu ikitajwa kuwa ina miaka zaidi ya 17,000.
Michoro mingi ni ya wanayama wakubwa wakubwa ambao wanatajwa waliishi miaka hiyo katika maeneo hayo. Mapango hayo yameorodheshwa na kutambulika na Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama urithi wa dunia.
Hata hivyo toka mwaka 2008 mapango hayo yamefungwa kutokana na mlipuko wa fangasi wanaotoko kwenye mapango hayo. Wakiruhusiwa wasayansi wachache sana angalau mara moja moja kwa mwezi kwa lengo la kutafiti.
2. Kisiwa cha North Sentinel, India
Ni kisiwa kidogo sana chenye msitu mnene zaidi kwenye ghuba ya Bengal. Ni moja ya visiwa vya Andaman kwenye bahari ya Hindi, kilichozungukwa na miamba mikubwa ya mawe ya matumbawe, hali inayoleta ugumu kukifikia kwa njia ya boti.
Lakini hicho sio kikwazo pekee cha watu kutoruhusiwa kufika ama kushindwa kutembelea, kikwazo kikubwa ni kwamba kisiwa hicho ni makazi ya watu wa jamii ya Sentinel ambao hawataki muingiliano na watu wengine duniani.
Inaelezwa ndio jamii iliyosalia duniani ambayo haijaguswa na maisha ya kileo na dunia ya sasa.
Mwaka 2008, wavuvi wawili ambao boti yao kwa bahati mbaya ilikaribia kisiwa hicho waliuawa na watu hao. Na mwaka 2004 wakati wa dhoruba kubwa la Sunami, wanasayansi walitumia helkopta kuangalia athari zilizowakumba watu hao. Wakiwa kwenye anga za fukwe walianza kushambuliwa kwa mishale, mikuki na mawe.
3. Doomsday Vault, Norway
The Doomsday Vault ni benki ama ghala kubwa la mbegu duniani, linalopatikana nchini Norway. Kila mbegu unayoijua duniani na kutumika kwenye kupata zao inahifadhiwa hapo.
Ghala hili liko mbali na makazi ya watu na mahala ambapo hata vita ikitokea ama gharika lolote likitokea mbegu hizo zitaendelea kuwa salama.
Sehemu kubwa ya ghala hilo iko ardhini na haifikiki kirahisi labda kwa watumishi wachache wanaofanya kazi hapo. Ni eneo lenye baridi sana na kulindwa wakati wote.
4. Poveglia, Italia
Kisiwa kingine kidogo kinachopatikana kati ya Venice na Lido kaskazini mwa Italia. Katika historia ya kisiwa hicho, ni mahala panapopatikana sana ngome kongwe , mahala ambapo palitumika kama kituo cha kuangalia usalama wa meli na baadaye pakatumika kama karantini ya kuwahifadhi wagonjwa wenye magonjwa mbalimbali hasa ya mlipuko na magojwa ya akili.
Lakini mwaka 1968, hospitali iliyokuwa inatumika kwa wagonjwa hao ambao wengi walikuwa wenye magojwa ya akili, ilifungwa na tangu wakati huo, kisiwa hicho kimetelekezwa.
Kuna hisia kwamba tangu kufungwa kwa hospital hiyo, mizimu ya wagonjwa waliofariki, watu waliouawa kweye vita inaendelea kuwepo kwenye majengo ya kisiwa hicho. Kumedaiwa kuwepo kwa sauti zikisikika kwenye miamba na mawe yaliyoporomoka.
Sauti zisizoeleweka. Watu wengi walikacha kwenda kwa hofu. Mwaka 2014 Serikali ya Italia iliwahi kutangaza kukipangisha kisiwa hicho kwa miaka 99 ili kuvutia watu watakaokiendeleza, lakini hofu imetawala zaidi ya kufika huko.
5: Kisiwa cha Nyoka, Brazil
Kama jina lake lilivyo, Kisiwa cha nyoka chini Brazil (Ilha da Queimada Grande) ni eneo lenye nyoka wengi na wakali pengine kuliko maeneo yote duniani yenye ukubwa huo.
Ni eneo lenye ukubwa wa hekari 43 na nyoka wanaopatikana wanatajwa kuwa na sumu kali zaidi na inayoweza kuua binadamu kwa haraka.
Kila mita za mraba tano kuna nyoka, ni sawa na hatua kama tano ukitembea kwa miguu lazima ukutane na nyoka wa ukubwa tofauti.
Utafiti unaonesha kuna nyota zaidi ya 4,000 aina ya Golden Lancehead Viper wanaopatikana kwenye kisiwa hicho kilichoko maili takribani 20 kutoka pwani ya mji wa Sao Paulo.
Serikali ya nchi hiyo imepiga marufu binadamu yeyote kutembelea kisiwa hicho kwa sababu ya usalama.
Wanasayansi wachache tena kwa tahadhari kubwa na nyenzo za kisasa za kujilinda wamekuwa wakiruhusiwa kufanya utafiti kila baada ya miaka mitano tena kwa vibali maalumu vya kufa ama kupona.