Sunday, November 24

AHMAD AL-FALASI FOUNDATION KUSAIDIA ZANZIBAR KATIKA SEKTA YA AFYA

Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Dkt. Msafiri Marijani (kushoto) wakimtembeza Mfadhili Ahmad AL- Falasi katika maeneo mbalimbali ya Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja kuona changamoto zilizopo.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Dkt. Msafiri Marijani akizungumza na Mfadhili kutoka (UAE) Ahmad AL- Falasi (wakwanza kulia) akiwa na familia yake walipofika Ofisini kwake Mnazimmja Hospitali.

Ahmad AL- Falasi ambae ni Mfadhili kutoka Dubai anaetaka kusaidia Zanzibar katika sekta ya afya akizungumza na wazazi wa wagonjwa alifika  haspitali ya mnazimmoja kupata huduma ili kuona changamoto zinazowakabili.

Ahmad AL- Falasi ambae ni Mfadhili kutoka Dubai anaetaka kusaidia Zanzibar katika sekta ya afya akizungumza na wazazi wa wagonjwa alifika  haspitali ya mnazimmoja kupata huduma ili kuona changamoto zinazowakabili.

Ahmad AL- Falasi na ujumbe wake wakitembezwa katika Kitengo cha Usafishaji Damu kwa wagonjwa wa Figo ambapo ameahidi kujenga kituo kama hicho kisiwani Pemba.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akiwa katika picha ya pamoja na wageni wake

Picha na Makame Mshenga.

Na Rahima Mohamed Maelezo 

Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui amepokea ugeni kutoka falme za kiarabu wenye lengo la kuisaidia sekta ya afya katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha sekta hiyo.

Waziri Mazrui amesema ugeni huo umeahidi kukiimarisha  kitengo cha usafishaji damu kwa wagonjwa wa maradhi ya figo pamoja na  kujenga kituo chengine kama hicho huko kisiwani  Pemba.

Ameyasema hayo wakati ugeni ulipofanya ziara ya kutembelea Hospitali Rufaa ya Mnazi Mmoja na kukagua vitengo mbalimbali vilivyomo katika hospitali hiyo na kuona changamoto zilizomo.

Amesema kitengo usafishaji damu kwa wagonjwa wa maradhi ya figo kina mahitaji muhimu sana ambayo yana gharama kubwa hivyo ugeni huo uko tayari kukisaidia kitengo hicho kwa kukipatia mafunzo madaktari pamoja na vifaa tiba.

“Katika ziara hiyo wameona changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hii hivyo ameahidi pia kuzifanyia  kazi na kusaidia  changamoto hizo na  kutafuta wafadhili ikiwemo wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji wa maradhi ya mifupa”, alieleza Waziri Mazrui.

Kwa upande wake Ahmad Al-falasi Foundation amesema yuko tayari kuisaidia Zanzibar katika sekta ya afya na kuweka vifaa vipya pamoja na kuwapatia mafunzo wafanyakazi hao .

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Mnazi Mmoja Dkt. Msafiri Marijani amesema ujio huo utaleta faraja kubwa katika upanuzi wa hospitali hiyo kutokana na majengo yake kuwa ya zamani na kusababisha kukosekana kwa baadhi ya huduma kufanyika kwa ufanisi zaidi.