Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa ametoa pongezi kwa Kampuni ya DSTV Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia Tasnia ya Filamu nchini kupitia Chaneli zao
Waziri Bashungwa amesema hayo alipokutana na Viongozi wa DSTV leo Julai 5, 2021 Jijini Dar es Salaam ikiwa ni ziara ya kuendeleza mahusiano kati ya Wizara na Kampuni hiyo
“Mimi nawapongeza DSTV kwa kuwa mstari wa mbele katika kukuza sanaa yetu ukizingatia mmeweka Chaneli ya Maisha Magic Bongo kwaajili ya filamu na tamthiliya za kitanzania tu hii ina manufaa sana kwa wasanii wetu kama dada yangu Lamata hapa kaweza kujiajiri na kuwaajiri Watanzania wenzie wengi kama waandishi wa miswada, wapiga picha na wasanii kwa ujumla hii yote ni kutokana na DSTV kutoa mwanya kwa wasanii wetu kuonyesha kazi zao” amesema Mhe.Bashungwa.
Mhe.Bashungwa ameongeza kuwa Kampuni hiyo imesaidia kukuza lugha ya Kiswahili katika Bara la Afrika na Dunia.
Hata hivyo Waziri Bashungwa ameiagiza COSOTA kufanya msako mkali kwa wezi wa kazi za wasanii nchini hasa wasambazaji wa Cable TV mikoani ambao hujiunga kiholela na kusambaza kwa wateja ambao hawaingizii mapato Kampuni na Serikali.
‘Swala hili la wezi (Pirates) wa maudhui na kazi za wasanii naagiza COSOTA na BASATA kusimamia kisawa sawa na kuwachukulia sheria haraka iwezekanavyo na nasikia kesi mnazo na wanajulikana na ushahidi mnao sasa naomba niwaagize mkalifanyie kazi hili maana hawa ndiyo wanao dhorotesha tasnia na wasanii kwa ujumla hata mapato serikali inakosa maana wanatumia njia zisizo sahihi”amesisitiza Mhe.Bashungwa.
Katika kikao hicho Mkurugenzi mtendaji wa DSTV Jacqueline Woiso amemshukuru Waziri Bashungwa kwa kutembelea ofisi hizo ambapo amemuomba kusaidia kutatua changamoto za Chaneli za bure za kitanzania kwakuwa ni kikwazo kikubwa kwao kupata wateja, Na Mhe. Bashungwa ameahidi kutatua changamoto hiyo.