Jina la Lulu Abas Silangwa maarufu Lulu Diva linapotajwa hasa nchini Tanzania, wengi watamtambua hasa vijana . Je ni kwanini?
Lulu Diva ni msanii wa Tanzania aliyejipatia umaarufu kutokana na mtindo wake wa maisha ambao umeibua hisia mseto. Wale wanaomthamini na kumuenzi wanafanya hivyo kwa asilimia 100, na wale wenye maoni tofauti kuhusu usanii wake pia wanafanya hivyo kwa kwa asilimia mia moja.
Hata hivyo hilo halimkoseshi usingizi Lulu ambaye anasema kuwa ndoto yake ya kuwa mwanamuziki bora, muigizaji anayebobea kwenye fani yake na vilevile mjasiriamali inamsukuma kila siku kutaka kufanya vizuri na kwa ubora, hayo mengine kwake ni hadithi tu.
“Tangu nikiwa binti, nilikuwa na ndoto kubwa za kufikia makubwa katika utu uzima wangu kwa mfano nilikuwa nataka kuwa mwanamuziki mkubwa hali kadhalika muigizaji. Hiki ndicho kitu ambacho nimeanza kukifikia ila hatua kwa hatua “Lulu anasema
Safari ya mwanadada huyu mzaliwa wa Tanga imekuwa na pandashuka nyingi, ila anasema kuwa pandashuka hizo zimemtayarisha katika kupigania nafasi yake kama msanii wa kike.
CHANZO CHA PICHA,LULI DIVA
Bi Lulu anasema maisha yake ya utotoni yalikuwa ya kawaida wakati huo baba yake mzazi akiwa hai, lakini mambo yalibadilika baada ya baba yake kufariki dunia. Cha kwanza kilichokwenda kombo ni uwezo wa mama mzazi kumsomesha.
“Wakati baba yangu alipoaga dunia nilikuwa naingia kidato cha pili , ilibidi mama atafute mdhamini ambaye alikuwa anaishi jijini Dar es salaam , kwa hiyo ilinibidi nitoke Tanga nyumbani kwetu hadi jijini Dar es salaam na kuendelea na masomo yangu .”anakumbuka Lulu.
Anasema jitihada zake katika shule Sekondari zilimwezesha kuchaguliwa kushika nyadhifa za uongozi wa wanafunzi, hali kadhalika alijihusisha mno na masuala ya Sanaa shuleni.
Baada ya kukamilisha masomo ya Sekondari , ilikuwa wazi kuwa kama mtoto wa kipekee kwa upande wa mama yake ilimlazimu aanze kusaka ajira . Alipata kazi kama muhudumu wa baa moja jijini Daresalam.
Haikuwa rahisi kama binti kutokana na unyanyapaa unaowakumba wanawake wanaohudumu katika migahawa au baa.
Mwanadada huyu anasema kuwa jinsi jamii inamtizama mwanamke aliyeko kwenye ajira ya mhudumu inakuwa ni ya kushusha hadhi ya utu wa mtu. Ila alikaza kamba kazini kuhakikisha kuwa yeye na mama yake wanaishi maisha ya kawaida.
CHANZO CHA PICHA,LULU DIVA
Kwa mfano anasema kuwa wamiliki wa baa au maeneo ya vilabu au migahawa wanakuwa wanatilia maanani sana biashara zao ili kupata faida kuliko hali ya wafanyakazi wake.
Vile vile anasema kuwa mshahara wa wahudumu wa maeneo haya wanalipwa mshahara mdogo kuliko bakshishi (tipu) ambayo wanapata kutoka kwa wateja wanaowahudumia kwa vinywaji na vyakula mbalimbali.
“Wakati huo nafanya kazi kama mhudumu nilikuwa sina chochote hadi nilikuwa naishi na rafiki yangu mmoja, na wakati nilianza kuwa na uwezo wa kuishi pekee yangu nilianza kuishi eneo la Tandale katika nyumba za uswahilini zilizokuwa zinapangishwa kwa bei ya chini kiasi kuwa ningeweza kumudu . “anakumbuka Lulu.
Lakini anasema kuwa tukio mmoja ambalo hatalisahau katika kazi yake hii ya kuwa mhudumu ni pale aliposhambuliwa na mteja.
Je ni nini kilitokea?
“Tukio hilo lilifanyika kwa haraka sana, huyo mteja alikuwa ameagiza kinywaji baridi lakini baadae akadai alikuwa ameagiza kinywaji moto. Kwa kuwa tayari nilikuwa nimefungua kile kinywaji nilijaribu kumshawishi akubali kinywaji hicho la sivyo ingenilazimu mimi nilipe nasikuwa na hela. Mara ghafla yule mteja alinizaba kofi la ajabu, ambalo sitawahi kusahau”, Lulu aliniambia.
Katika kipindi hicho Lulu aliona umuhimu wa kusomea taaluma ya hoteli na aliingia katika taasisi ya mafunzo ya kazi ya hoteli , ili awe na nafasi nzuri zaidi za kazi kuliko aliyokuwa nayo.
Vile vile Lulu anasema kuwa hakufa moyo katika kufanikisha ndoto yake ya kuwa mwanamuziki, muigizaji na pia mfanyabiashara.
CHANZO CHA PICHA,LULU DIVA
Kwa hivyo kila nafasi aliyoipata ya kuonyesha talanta yake kwa waliomtangulia katika fani hiyo aliitumia kwa busara.
Jina la Lulu Diva kisanii lilianza kutamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa udi na uvumba kama anavyosema amepigania nafasi yake kama mwanamuziki na muigizaji.
“Haikuwa rahisi kwangu kuafikia kuwa msanii mkubwa hapa Tanzania, kwanza kabisa kuna dhana nyingi ambazo zinahusishwa na wasanii wa kike, hasa jinsi tunavyofika kwenye majukwaa makubwa ya usanii , ila mimi naamini kuwa ni jasho langu na ari ya kuendeleza talanta yangu imenifikisha nilipo”, Lulu anasema.
Kuugua kwa mama yake
Tukio ambalo limekuwa pigo kuu katika maisha yake, lilianza miaka tisa iliyopita wakati mama yake mzazi alipoaanza kuumwa ugonjwa ambao ulimuathiri kiakili.
Tangu wakati huo hadi wa leo Lulu anasema mama yake mzazi hajazungumza wala kutembea mwenyewe.
Kilio kikuu cha msani huyu ni kuwa wakati anaanza kupata kipato cha kumuwezesha yeye na mama kuishi maisha ya stara kuliko maisha ya taabu walikotoka, ndio wakati mama yake alianza kuumwa ugonjwa ambao umekuwa ukiwasumbua kwa muda mrefu.
“Mama hajazungumza kwa miaka tisa, sijui anafikiria nini?, sijui ananiwazia yepi na hata sielewi yuko katika dunia ipi? Ni jambo linalonikosesha usingizi. Najiuliza na usanii huu wangu mama hajaweza kunishabikia kwani haelewi kinachofanyika, inauma sana kumuona mama akiwa katika hali hii.”Lulu anasema
Kwa miaka tisa hii, Lulu hajaweza kuzungumza na mama yake, na hata akimzungumzisha kutokana na maradhi yake hana uwezo wa kujibu, na Lulu hajui kama anatambua ama hatambui akizungumzishwa. Hilo linamtatiza sana Lulu.
Lulu anasema anajivunia mwaka 2018 kupitia kipato chake cha uanamuziki aliweza kumpeleka mama yake hospitalini alikofanyiwa upasuaji sehemu ya kiuno, lakini baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini , mama alipata ajali na akavunjika mguu wake tena. Tatizo juu ya tatizo.
Kaamua Kumtungia Wimbo Mama yake ‘Mama’
Mwanadada huyu anasema kuwa ugonjwa wa mama yake umekuwa ni mtihani mkubwa kwake , mwezi Aprili mwaka huu wa 2021 akaamua kumuandikia wimbo maalumu wenye historia yake na mama yake mzazi.
Wimbo huyo unaoitwa MAMA, ni maalumu kwa ajili ya mama yake – kwenye wimbo huo unaoibua hisia ya huruma anatoa ujumbe wa maombi yake kwamba siku mmoja mama yake atazungumza na kutembea tena. Wimbo huo wa Lulu Diva umesikilizwa na kutizamwa kwa wingi katika mtandao wa Youtube.
Kwenye wimbo huu Lulu anasema nikimnukuu “Hii ni kutoka moyoni, nakupenda mama, na ndio sababu kutwa napambana , kinachonitesa moyoni unaumwa sana , ila naamini ipo siku utapona, maana huwezi kula mwenyewe , wala kutembea mwenyewe pengine ni siri yangu mwenyewe ” ujumbe katika sehemu ya wimbo huo wa mama unasema.
Kwenye video ya wimbo huu, anaonekana mama yake akiwa kitandani.
Lulu Diva aliyezaliwa kama mtoto wa pekee anasema kuwa ametambua umuhimu wa kuwa na jamii na haja ya kujaaliwa na watoto.
Katika mitandao ya kijamii Lulu ni mmoja wa wasanii ambao pia wameibua gumzo juu ya masuala mbalimbali hasa ya mahusiano na mtindo wake wa maisha.
Akijibu baadhi ya tuhuma hizo, Lulu anasema kila mtu ana mtindo wake wa maisha, na hawezi kwenda kila mahali na kujitambulisha kuwa yeye ni nani kiuhalisia