Tuesday, November 26

Mdhamini akabidhi vifaa vya kilimo.

AFISA Mdhamini Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba, Fatma Hamad Rajab akiwakabidhi kamba na vifaa mbali mbali vya kilimo, wanakikundi cha shumba Viwamboni kwa ajili ya shuhuli zao za kilimo.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

AFISA Mdhamini Wizara ya Vijana Utamaduni sanaa na Michezo Pemba, Fatma Hamad Rajab amekabidhi vifaa mbali mbali vya kilimo kwa vikundi sita vya vijana kutoka Wilaya nne za Pemba.

Makabidhiano hayo ni utekelezaji wa program ya ajira kwa vijana ya Bilioni 3, ilianzishwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa vikundi hivyo vya kilimo, Afisa Mdhamini huyo aliwataka wanavikundi kuthamini juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuwasaidia, kuondokana na utegemezi wa ajira kutoka serikalini.

Alisema serikali ya awamu ya samba, imeweza kuwafanyia mambo mengi mazuri ikiwemo kuanzishwa kwa program ya ajira kwa vijana, ambayo imekuwa ikiwasaidia vitu mbali mbali vya kujiajiri wenyewe na kutokutegemea ajira serikalini.

“Mwanzo wa programa hii tulitoa vifaa vya kilimo na ushoni kwa vikundi vyetu na mara hii pia tumetoa kama hivyo sasa ni wajibu wenu kuonesha fadhila kwa serikali yetu juu ya msada wao”alisema.

Aidha aliwataka kuhakikisha wanavitumia ipasavyo vifaa hivyo,  kwani hatokuwa tayari kuona vikundi vinashindwa kuthamini mali ya serikali, kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwapokonya mali hizo.

Hata hivyo alisema wakati umefika kwa viongozi wa vikundi hivyo, kutokuwa nyuma na badala yake kubadilika katika shuhuli zao za kilimo, kwa kulima vilimo vinavyoendana na mabadiliko ya dunia ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.

“Vizuri katika kuzalisha mazao tukaangalia vile vitu ambavyo havijalimwa na watu wengi, wapo wenzetu wamelima vitunguu maji mara hii”alisema.

Kwa upande wake Mratib wa Idara ya Vijana Pemba, Ali Mussa Bakari alivitaja vifaa mbavyo vimekabidhiwa kuwa ni pamoja na mbolea polo 12, vifaa vya umwagiliaji maji kwa matonye 12, mapanga 18, mota za kusukumia maji 5, Reng buti 18, majembe 15, Trea za kuoteshea miche 60, dawa za viwatilifu 36, mpira wa maji mita 47 kila kikundi na kamba 24.

Aidha aliwataka viongozi wa vikundi hivyo kuhakikisha vifaa hivyo wanavitumia kwa lengo lililokusudiwa, pamoja na wizara kuvifuatilia matumizi yake.

Katibu wakikundi cha Nia Yetu kutoka Mgogoni Konde, Hamad Said Hamad alisema vifaa hivyo kwao vimefika kwa wakati muwafaka, kwani vitaweza kuwasaidia katika shuhuli zao za kilimo.

Hamad Omar kutoka kikundi cha kilimo Hai Chamanangwe, aliishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapatia vifaa hivyo, huku akiahidi kutumika kwa lengo lililo kusudiwa.