NA ZUHURA JUMA, PEMBA
“RUSHWA muhali, kutojiamini, kupotea malezi ya pamoja ni visababishi vikubwa vinavyopelekea kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji ndani ya jamii”, hayo ni baadhi ya maneno ya wanajamii Wilaya ya Wete.
Mwandishi wa makala haya aliwafikia wanajamii mbali mbali kwa lengo la kujua vyanzo vinavyosababisha kuongezeka kwa udhalilishaji , ambapo Katija Mbarouk Ali mkaazi wa Kiuyu Kigongoni anaeleza kuwa, zipo sababu mbali mbali zinazopelekea kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya udhalilishaji.
Anasema, zamani kulikuwa na malezi ya pamoja ambayo hushirikiana wazazi wa mtaa kuwalea watoto, jambo ambalo lilisaidia sana kuwatunza na kuwalinda watoto.
“Kwa sasa kila mzazi analea mtoto wake pekee na anapofanya kosa ukimwambia anakuwa mkali, hivyo hata ukimuona mtoto na uovu gani watu wananyamaza kwa sababu wanaogopa kutukanwa”, anaeleza Katija.
Anasema, malezi ya pamoja ndani ya jamii ni muhimu sana na ndio ngao pekee itakayopunguza wimbi la udhalilishaji, hivyo ipo haja ya kuyarudisha ili watoto wawe salama.
Anakumbuka Saada Ali Said mkaazi wa Madenjani Wilaya ya Wete kwamba, malezi yaliyokuwepo yalisaidia sana kulinda mbaya asipate nguvu ya kuwaharibu watoto kutokana na umoja uliokuwepo baina ya mzazi na mzazi kwa vizazi vyao.
Anafahamisha kuwa, watoto katika kijiji enzi hizo walikuwa wakifanya kosa wakipewa hukumu na mzazi yoyote na sio mzazi wake tu na hakukuwa na kesi yoyote iliyokuwa ikiendelea baada ya mtoto wao kupewa hukumu kwa kosa alilofanya.
“Lakini hivi sasa hakuna mzazi aliye tayari kupambana na hiyo hali kama ambavyo wakifanya babu wa mababu zetu, kutokana na kila msemo unaotumika wa sasa kwamba kila mzazi atalea mwanawe ndio hayo yanarotudhuru na kusababisha kukua kwa matatizo mengi ndani ya jamii zetu”, anahadithia.
Anaeleza, maisha ya sasa hakuna anayetaka kulelewa mwanawe, hakuna anaethubutu kumuhukumu wala kumkanya mtoto wa mwenzake kwa kuogopa kufunguliwa kesi mahakamani.
Anasema, pia mzazi huogopa kurudishiwa kipigo kutoka kwa wanafamilia ya mtoto aliyepewa hukumu.
Mkaazi wa Kangagani Asha Hamad Ali anaeleza kuwa, kushamiri kwa matukio ya udhalilishaji ni kutokana na wazazi wenyewe kuacha utamaduni uliokuwepo hapo zamani na kufuata tamaduni za kimagharibi.
“Ili tatizo hilo liweze kuondoka ipo haja ya kurejesha malezi ya pamoja kama ambavyo walikuwa wakifanya wazazi wetu”anaeleza.
Mwananchi huyo pia aliomba zile sheria zilizowekwa zitumike ipasavyo, ili kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa maslahi ya jamii na taifa.
Nae mzazi wa mtoto ambaye alifanyiwa vitendo vya udhalilishaji jina limehifadhiwa anaelezea kuwa, tatizo kubwa linalopelekea vitendo hivyo kuongezeka ni kutokutumiwa kwa sheria ya kuwakamata mashahidi ambao hawataki kutoa ushahidi pale wanapohitajika mahakamani.
“Kutokana na tabia mbaya inayoendelea kwa baadhi ya watu kujifanya hawataki kwenda mahakamani kutoa ushahidi kwakuhofia kurogwa ama kutengwa, husababisha kuongezeka kwa vitendo hivyo kwani watuhumiwa hupata nguvu”, anafafanua.
Alieleza kuwa, ili tatizo liondoke, wachukuliwe hatua kali wale wote wanao kataa kutoa ushahidi, ili iwe funzo kwao na kwa wengine wenye tabia kama hizo, jambo ambalo litasaidia mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Mama huyo aliiomba jamii kuwa makini katika kusimamia kesi zao, kutoa mashirikiano kwenye vyombo vya sheria na kuwafichua wanaofanya na kujaribu kufanya udhalilishaji, ili kuwasaidia watoto kuwa salama na huru.
Fatma Hamad Ali mkaazi wa Chwale Wilaya ya Wete, anaelezea kwamba vitendo hivyo husababishwa na vyanzo vingi, ikiwemo rushwa ya pesa, ambayo hutumika kwa kuvunja kesi.
“Wapo baadhi ya watu waliowafanyia watoto udhalilishaji, lakini wakakubali kupokea pesa ili kesi ifutwe, hili ni jambo baya na kesi haiwezi kufika popote”, anasema.
“Vitendo vya udhalilishaji ni jambo linalopigiwa kelele kila siku kwa Serikali pamoja na taasisi binafsi, lakini bado jamii yenyewe inaonekana haipo tayari kuunga mkono nguvu hizo”, anaeleze.
Lengo la Serikali ni kuona jamii inaunga mkono juhudi mbali mbali zinazochukuliwa katika kupambana na vitendo hivyo, ili kuondosha kabisa tatizo hilo.
“Tujue kwamba suala la kupinga udhalilishaji ni jukumu la kila mtu na sio la mmoja pekee ama taasisi fulani, kila mtu mwenye akili timamu ana haki yakushiriki kupambana na kuwafichua wahalifu bila kuwaonea aibu, ili kusaidia kizazi chetu kufikia ndoto zao za kimaisha”, anaeleza Ali Shehe Khamis mkaazi wa Mchangamdogo.
Ameshaona kesi nyingi zinamalizia kwenye familia na hatimae mtoto kubaki nyumbani na kulea mwanawe baada ya kuzaa bila kupata huduma yoyote, ambapo wengine huishia kuwa ombaomba.
Anafahamisha kuwa, kinachoonekana kwa baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamefikwa na kadhia hiyo ni kukubali kupokea rushwa, ili tu kesi isifikshwe mahakamani jambo ambalo linazidi kumuathiri mtoto hadi anafikia utuuzima.
Mkaazi wa Kidutani Ali Said Khamis anasema, ipo haja kwa vyombo vya sheria ikiwemo Mahakama, Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka, kuwachukulia hatua kali wazazi watakao kataa kutoa mashirikiano kwa kuhofia kutengwa.
“Kutokana na kuwa katika jamii huendelea kufanywa matukio ya kusikitisha na kumaliza kesi hizo kifamilia, ipo haja ya kuchukuliwa hatua kwani sheria hizo zipo hivyo zifanyiwe kazi”, anafahamisha.
Wazazi walieleza kama ni kweli wapo baadhi ya wazazi wenzao hujifanya mahakimu kuhukumu kesi hizo kifamilia kwa kuhofia kurogwa na kutengwa na majirani zao, bila kuona kwamba wanazidi kumuathiri mtoto wao.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Ofisi ya Pemba Fathiya Mussa Said anasema kwamba, bado vitendo vya udhalilishaji ndani ya jamii ni gumzo, ambalo lipo kila pembe, licha ya jitihada Serikali na taasisi binafsi juu ya elimu inayotolewa.
Anafahamisha kuwa, licha ya elimu na mafunzo wanayopatiwa wanajamii lakini kumeonekana hakuna mabadiliko, hivyo kuna haja ya kuongeza bidii ili watu waelewe zaidi.
Mwendesha mashitaka Juma Ali Juma anasema, elimu imeshafikishwa kwenye jamii na wanafahamishwa jinsi ya kupambana na vitendo hivyo, ingawa bado wajamii wanaonekana hawana msimamo katika kusimamia kesi zao ipasavyo.
Kinachosikitisha ni kumuona mzazi ama mtoto kujifanya na aibu na kukataa kutoa mashirikiano pale wanapohitajika kutoa ushahidi, jambo ambalo linapelekea kesi kufutwa kwani bila ya ushahidi hakuna hatia.
“Kesi yoyote ikiwa haina mashirikiano yakutosha haiwezi kufikia lengo na baadae hao hao wazazi hupeleka lawama na kuisema Serikali kwamba haifanyi haki na wakati wao wenyewe hawako tayari kuunga mkono juhudi hizo”, anafahamisha.
Hiyo ni moja ya changamoto ambazo hukumbana nazo na kuwafanya wabaki katika wakati mgumu wa kufikiria jinsi ya kuitatua, ili kesi hizo zipate hatia.
Abdalla Yahya Shamhun ambae ni hakimu wa Mahakama ya Mkoa Wete anaitaka jamii iondokane na dhana potofu ya kwamba vitendo hivyo vinachangiwa na hali ngumu ya kimaisha na badala yake wawe na msimamo wa kusimamia mashauri yao hadi haki ipatikane.
“Dhana ya umasikini isiwe chanzo cha kuzorota kwa kesi, wawe tayari kusimamia na kufuatilia mpaka haki itakapopatikana”, anafahamisha.
Aliishauri Serikali kutenga bajeti ya fedha itakayosaidia familia yenye hali ngumu katika kufuatilia kesi zao, ili isiwe kikwazo cha kutofika mahakamani kutoa ushahidi.
Hakimu Shamhun aliitaka jamii kujua kwamba, haki inapatikana mahakamani na siyo kwenye familia, hivyo atathubutu kusuluhisha kesi za udhalilishaji ajue kwamba anachangia kuongezeka kwa vitendo hivyo.
“Na ndio maana Dk Mwinyi ameanzisha mahakama maalumu zitakazoshuhulikia kesi hizo tu, kwa hiyo jamii nayo iunge mkono jitihada za Rais, ili kuhakikisha tunafanikiwa mapambano”, anasema.
Mkuu wa dawati la jinsia mkoa wa Kaskazini Pemba, Fakih Mohamed Yussuf, anasema familia zenye tabia ya kusuluhisha kesi za udhalilishaji kwa kuhofia kusemwa ama kutengwa basi wajue kwamba watoto wao wanaendelea kudhalilishwa.
“Wazazi wanaojifanya mahakimu waache mara moja, hilo sio jambo zuri kwani wanapalilia vitendo hivyo kuongezeka siku hadi siku”, anaeleza.
Aliiomba jamii inashirikiana na vyombo vya sheria kuhakikisha wanapambana na wahalifu, kwa kuwafichua na kuwa mstari wa mbele kutoa ushahidi, ili kesi zipate hatia.
Tatu Abdalla Mselem ambae ni mratibu wa Jumuiya ya Tumaini Jipya anasema, kila mmoja kwa nafasi yake ambane ili kuondoka na janga hilo ambalo linamaliza Watoto.
“Watoto wanaumia, hawana raha, muda wote wana hofu, hivyo sisi wazazi ndio tutakaowasaidia watoto wetu, hivyo tuwalinde na kuwa nao karibu”, anasema.
Kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anapambana vikali, ili kufanikiwa kuondosha janga la udhalilishaji.