Tuesday, November 26

Mke wa rais: Mfahamu Angeline Ndayubaha Ndayishimiye mke wa rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye

Ni watu wenye ushawishi katika uongozi wa kila siku wa nchi zao, hata hivyo si kila siku utasikia juu ya maisha yao na vipawa vyao. Hawa ni wenza wa marais, ambao baadhi yao ni wanasiasa na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega katika safari za kisiasa za wenza wao mpaka kushika hatamu za madaraka. Wiki hii tunakuletea mfululizo wa makala kuhusu wenza wa marais katika eneo la Afrika Mashariki tukianza na mke wa Rais wa Burundi.

Kama ni kuwa muasi, mke wa muasi na mkimbizi, na hatimaye kuwa mke wa rais, basi ni maisha anayoyafahamu Bi Angeline Ndayishimiye, mkewe rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye.

Bi Angelina Ndayishimiye ni nani hasa ?

Angeline Ndayubaha Ndayishimiye alizaliwa tarehe 18 Juni 1976 katika eneo la Kiganda katika wilaya ya Muramvya, nchini Burundi ambako alipata elimu yake ya msingi na sekondari.

Ukilinganisha na wake wengine wa marais, taarifa kuhusu maisha yake binafsi yake kabla ya kuolewa na Evariste ni nadra.

Angeline Ndayishimiye/Twitter

CHANZO CHA PICHA,ANGELINE NDAYISHIMIYE/TWITTER

Maelezo ya picha,Picha ya Bi Angeline Ndayubaha Ndayishimiye kabla ya kuwa mke wa Rais, akiwa msituni

Hata hivyo taarifa kuhusu maisha yake ya awali zimeanza kujitokeza baada ya kuwa mke wa rais Evariste Ndayishimiye.

Aliolewa na Bw. Ndayishimiye ukimbizini na baada ya mumewe ambaye alikuwa mkimbizi na muasi kuyakimbia machafuko ya kikabila alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Burundi na kujiunga na kikundi cha waasi cha (CNDD-FDD), ambacho kilipata uungwaji mkono kutoka kwa watu wa jamii ya Wahutu.

Wawili hao walioana wakiwa wakimbizi na wamejaaliwa watoto wanane.

Bi Angeline Ndayishimiye Nayishimiye na Rais Ndayishimiye wamejaliwa watoto wanane

CHANZO CHA PICHA,NTARE RUSHATSI

Maelezo ya picha,Bi Angeline Ndayishimiye Ndayubaha na Rais Ndayishimiye wamejaliwa watoto wanane

Mumewe Jenerali Evariste Ndayishimiye (almaarufu Neva) alikuwa miongoni mwa wanajeshi waasi wa CNDD-FDD waliopigana vita dhidi ya utawala wa Pierre Buyoya kuanzia miakaya 90 hadi mwaka 2003 ambapo alikuwa pia Katibu Mkuu wa chama hicho kuanzia mwaka 2016. Wakati huu wote Bi Angeline Ndayishimiye pia alikuwa muasi pamoja na mume wake.

Hata hivyo baada ya kuwa mke wa rais, Bi Angeline Ndayishimiye alituma picha kwenye mtandao wa Twitter zinazoonesha hali halisi ya maisha yake ya awali, zinazoaminiwa kuwa alizichukua wakati alipokuwa mke wa muasi, wakati wa utawala wa Pierre Buyoya miaka ya 2000.

Katika picha hizo alizozituma kwenye ukurasa wake wa Twitter, Bi Angeline anaonekana akiwa katika maeneo ya mapambano na kwenye maelezo ya picha hizo anasema: Nilikuwa mtafutaji wa amani nitaendelea kuwa mtafutaji wa maendeleo Burundi.

Aliporejea nchini kutoka ukimbizini kufuatia serikali ya Pierre Nkurunziza kuingia madarakani, Bi Ndayishimiye alianzisha wakfu unaofahamika -mwanamke shujaa ”femme Intwari”, uliowaleta pamoja wanawake ambao ni wapiganaji wa zamani pamoja na wake wa wapiganaji wa zamani kwa ajili ya kuhamasisha watu kuhusu umuhimu wa amani na demokrasia nchini Burundi.

Angeline Ndayubaha Ndayishimiye kama mke wa rais

Bi Angeline Ndayishimiye Ndayubaha alipata cheo cha mke wa rais wa Burundi rasmi tarehe 18 Juni, 2020 baada ya mume wake Evariste Ndayishimiye kuwa rais wa Burundi kufuatia ushindi wa uchaguzi na kuapishwa siku chache baada ya kifo cha mtangulizi wake Pierre Nkurunziza.

Angeline Ndayishimiye na Evariste Ndayishimiye (Neva), siku ya kuapishwa rasmi tarehe 18 Juni, 2020

CHANZO CHA PICHA,EVARISTE NDAYISHIMIYE/TWITTER

Maelezo ya picha,Angeline Ndayishimiye na Evariste Ndayishimiye (Neva), siku ya kuapishwa rasmi tarehe 18 Juni, 2020

Tangu wakati huo Bi Angeline Ndayishimiye alianza shughuli mbali mbali za ujenzi wa taifa, akishirikiana na mume wake.

Mwaka 2019 binafsi alianzisha kile kinachoitwa Wakfu wa matendo mema- Bonne Action -Umugiraneza mwezi wa Julai, 2019, lengo lake likiwa ni kuisaidia jamiii kwa vitendo, familia na watu binafsi na kuimarisha maisha ya wananchi kwa ujumla.

Kupitia wakfu huo ameweza kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo hususan ya wanawake, pamoja na utoaji wa misaada ya kiutu kwa raia masikini zaidi nchini humo.

Kupitia wakfu wa misaada wa Bonne Action, Bi Angeline amekuwa akizisaidia familia zisizojiweza zilizojaaliwa kupata watoto zaidi ya wawili kwa wakati mmoja:

Akifahamika na wengi kama mwanamke mchapakazi mke huyo wa rais ametokea kuwavutia Warundi wengi hasa wanawake kutokana na matendo yake yanayolenga kuinua maisha ya wanawake wenzake hususan katika sekta ya afya.

Kupitia Wakfu wake Bi Angeline Ndayishimiye Nayishimiye amefungua hospitali na kufuatilia ujenzi wa vituo vya afya kwa ajili ya matibabu ya akinamama na watoto katika maeneo mbali mbali ya nchi , mfano wa hivi karibuni ukiwa uzinduzi wa kituo cha matibabu ya Fistula mwezi Juni 2021, cha Gitega ili kuharakisha matibabu ya wanawake wenye Fistula ”femme Intwari”.

Chini ya wakfu huo pia Bi Ndayishimiye alifungua kituo cha kutoa ushauri wa kisaikolojia kilomita 70 kutoka mji wa Gitega ambapo vijana na watu wengine watapewa matibabu hayo na kusimamia ujenzi wa hospitali kubwa ya wanawake na watoto katiak eneo la Kimbiba.

Wanaomfahamu Bi Ndayishimiye wanamtaja kama mama mkakamavu, anayefahamu matatizo ya wananchi wa Burundi hususan wanawake na anayepigania maendeleo ya nchi.

Baadhi ya raia wa Burundi wamekuwa wakionesha hisia zao kumhusu Bi Ndayishimiye kwenye mitandao ya kijamii.

Katika mtandao wa Facebook Japhet Twagirayezu anasema: ”Endelea kutuongoza tunakufuata mama”

Patrick Kalabadumba anasema: ”Mungu aendelee kukuongoza, tunakupenda kwa shughuli unazozifanya kwa ajili ya ujenzi wa nchi”.

Tangu ashikilie cheo cha mke wa Rais Bi Angeline Ndayishimiye amekuwa akifanya ziara mbali mbali katika nchi za Afrika Mashariki na nje akiandamana na mume wake Evariste Ndayishimiye na anapokuwa katika ziara hizi, hujifunza mengi na kuanzisha ushirikiano wa kimaendeleo na wake wa marais wenzake pamoja na wataalam wa shughuli za kimaendeleo. Mojawapo ya ziara za hivi karibuni ikiwa ni ile aliyoifanya nchini Kenya akiwa na mume wake rais Evariste Ndayishimiye

Kauli zenye utata

Bi Angeline Ndayishimiye ni mwanamke ambaye anafahamika kwa kutotafuna maneno, hasa kwa kile anachokiamini.

Hali hii wakati mmoja ilimtia mashakani, tarehe 7 Septemba, 2020 pale alipotoa kauli zinazokinzana wakati wa mkutano na baada ya mkutano wa viongozi wanawake wa Burundi.

Katika hotuba rasmi ya ufunguzi wa mkutano huo, alisikika akiunga mkono usawa kati ya wanawake na wanaume akisema: “Tukumbushane kwamba Mungu aliyewapa akili wanaume aliwapatia pia wanawake. Mwanamke ana akili na uwezo wa kufanya mambo yoyote anayoweza kuyafanya mwanaume.”

Hata hivyo katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa YouTube wa Mashariki TV, baada ya hotuba ya kufungua mkutano, katika mazungumzo juu ya mahusiano ya wana ndoa, Bi Angeline Ndayishimiye anasikika akizungumzia juu ya usawa wa wanaume na wanawake. Anasema: “Haikuwahi kutokea, haitokei na haitawahi kuwa .”

Akitoa mfano wa kazi za nguvu alisema( kufungua ya maji ) wanawake hupenda kuwaomba wanaume wafanye kazi hiyo.

Anasema: “Huo ni mfano mdogo unaoonesha kuwa mambo ya wanaume na wanawake kuwa sawa kwanza msahau katika nchi ya Burundi, hilo halitakuwepo, ndio chanzo cha kutoheshimiana .”

Kauli hizi hazikuchukuliwa kirahisi na baadhi ya Warundi, likiwemo vuguvugu la Wanawake wanaopigania haki na usalama – Mouvement des Femmes et Filles pour la Paix & la Sécurité (MFFPS) lenye makao yake nchini Canada linalodai kuwa na wafuasi wengi ndani ya Burundi na kwingineko duniani.

MFFPS, lililaani kauli za mke wa Rais Ndayishimiye, likidai zinakwenda kinyume na katiba ya Burundi pamoja na sheria za kimataifa zinazosema “watu wote ni sawa mbele ya sheria”.

Haiba na muonekana

Tangu mume wake kuingia madarakani Bi Ndayishimiye amekuwa akionekana kwenye vyombo vya habari akitoa misaada ya mara kwa mara kwa watu masikini. Baadhi Warundi wanamuona kama mchapakazi, na mwenye huruma.

Angeline Ndayizeye Ndayubaha, akimnywesha soda mama mzee katika siku ya Wazee duniani tarere 1.10.2020

CHANZO CHA PICHA,ANGELINE NDAYIZEYE

Maelezo ya picha,Angeline Ndayizeye Ndayubaha, akimnywesha chupa ya maji mama mzee katika siku ya Wazee duniani tarere 1.10.2020

Hivi karibuni pia alivutia hisia za Warundi wanaotumia mitandao ya kijamii baada ya kuanzisha mashindano ya soka ya Kombe la Mke wa Rais, yaliyojumuisha timu timu 18 za wasichana. ” Vipaji vya wanawake vinapaswa kuthaminiwa”, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mtindo wake wa Mavazi

Kama ilivyo kwa wake wa marais wa nchi nyingine hususan za Afrika Bi Angeline Ndayishimiye Ndayubaha, ameonekana kuvaa mavazi ya heshima yanayoendana na mtindo wake wa nywele fupi zilizosukwa.

Mavazi yake ni pamoja na Suti za sketi na za suruali, nguo za kiafrika za batiki, pamoja na vazi la kitamaduni la kirundi ”imvutano”.

Angeline Ndayizeye

CHANZO CHA PICHA,ANGELINE NDAYIZEYE

Angeline Ndayizeye

CHANZO CHA PICHA,ANGELINE NDAYIZEYE

Angeline Ndayizeye

CHANZO CHA PICHA,ANGELINE NDAYIZEYE

Japokuwa ni mgeni katika nafasi ya cheo cha Mke wa Rais, akilinganishwa na wake wengine wa marais katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, ni dhahiri kwamba Bi Angeline Ndayubaha Ndayishimiye ameonesha kuwa mwanamke ambaye ana mwamko wa maendeleo ya wanawake na taifa la Burundi nyuma ya Rais Evariste Ndayishimiye.

Bi Ndayishimiye ni msomi mwenye shahada ya uchumi na utawala.

CHANZO CHA HABARI BBC