Saturday, October 19

SOS yakabidhi milioni 40 Tumbe.

 

SHIRIKA lisilo la kiserikali SOS Zanzibar limekabidhi hundi yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 40, kwa uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa kituo cha afya cha Tumbe wilaya ya Micheweni.

Hafla hiyo ya makabidhiano ya hudi hiyo, imefanyika katika ukumbi wa Mikutano Micheweni, huku ikihuduriwa na viongozi mbali mbali, wakiwemo watendaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni pamoja na viongozi kutoka SOS wakiwa na mjumbe wa bodi wa shirika hilo.

Akizungumza kabla ya makabidhiano hayo Mjumbe wa Bodi wa Shirika la SOS Zanzibar Dk.Issa Seif Saleh alisema lengo la kukabidhi fedha kwa ajili ya kumalizia kitengo cha mama na mtoto Tumbe.

Alisema kazi yao kubwa SOS ni kuwalinda watoto na kuwalea, kuwakuza na kuwapa maadili yote ili kuweza kuwaendeleza maisha yao ya baadae, ili kuweza kusaidia familia zao na jamii yao.

“katika kuwapa kipaombele watoto tumeona bora tuanze na kituo cha afya, watoto wanapokuwa na afya bora wanaweza kufanya mambo yao vizuri kwa asilimia kubwa”alisema.

Aliwataka kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja kuwafikia walengwa ni watoto, kuwaandalia malazi bora, afya bora na maadili ili waweze kufikia malengo yao.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Hamad Mbwana Shehe alilishukuru shirika la SOS kwa juhudi kubwa wanazozichukua katika kuunga mkono juhudi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwemo sekta ya elimu na afya.

Alisema SOS imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama, pamoja na kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu.

“Naweza kusema wananchi wa Tumbe wamekuwa na bahati ya pekee, katika shirika hilo kwani miradi mingi imeelekezwa kwao, lengo ni kuona watoto wanaishi katika maisha bora”alisema.

Aidha aliuhakikishia uongozi wa SOS kuwa msaada waliopatiwa watahakikisha wanautumia kwa lengo lililokusudiwa, ili akinamama na watoto waweze kupata huduma bora za matibabu kituoni hapo.

Hata hivyo mkurugenzi huyo aliwashukuru wananchi wa Tumbe, kwa akuanzisha ujenzi wa jingo jipya la kituo cha afya, kwa kushirikiana na Jumuiya ya maendeleo ya shehia ya Tumbe (JUMATU), baada ya kuona akinamama na watoto wanapata shinda.

Kwa upande wake Mratib wa shirika la SOS Pemba Gharib Abdalla Hamad, alisema lengo la kukabidhi msaada wa fedha hizo ni kwa ajili ya kuendeleza kituo cha afya ya mama na mtoto katika shehia za Tumbe mashariki na magharibi.

Alisema lengo la SOS ni kuona watoto wanaishi katika mazingira salama, ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya na malazi bora pamoja na suala zima la elimu.

Alisema matarajio ya SOS ni kuona watotoi wanapatiwa huduma za afya kituoni hapo, pamoja na wazazi kujifungulia sehemu sahihi baada ya kumalizika kwa ujenzi wake.

“Sisi SOS tumekuwa mstari wa mbele katika kusaidia harakati za wananchi wa Tumbe, yote haya yanafanyika kupitia mradi wetu wa kuimarisha familia”alisema.

Kwa upande wake msaidizi Mkurugenzi Utawala na uwendeshaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Ali Salum  aliishukuru shirika la SOS kwa kusaidia juhudi za jamii katika maeneo mbali mbali ya kisiwa cha Pemba.

“SOS ni shirika ambalo lipo mstari wambele katika kusaidia shuhuli za jamii,zipotaasisi nyingi ila SOS imekuwa mstari wamble”alisema.

Hata hivyo aliyataka mashirika mengine kujitokeza kuunga mkono juhudi zinazoanzishwa na wananchi, ili kuweza kufikia malengo yao waliojiwekea.

Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Tumbe (JUMATU) Nassor Suleiman Nassor, aliipongeza SOS kwa kuwa mstari wambele kuwasaidia wananchi wa tumbe, ili kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata.

Alisema kituo cha afya kilikuwa ndio kilio kikubwa kwa wananchi wa Tumeb, kwani hulazimika kutumia shilingi elfu 30,000/= kuwafikisha akinamama wajawazito Micheweni Hospitali.

Nao akinamama wa tumbe, wamesema kuwa kumalizika kwa kituo cha afya Tumbe, kitakuwa ni mkombozi mkubwa kwao pamoja na watoto wao.