Saturday, October 19

Wanafunzi wahimizwa kuendeleza usafi wa mazingira katika maeneo wanayoishi.

 

HABIBA ZARALI,PEMBA

WANAFUNZI wa skuli mbalimbali zilizojiunga na klabu inayojishughulisha na mazingira Kisiwani Pemba ‘Roots And Shoots’ wametakiwa kutojisahau na badala yake waendeleze kuhifadhi usafi wa mazingira katika maeneo wanayoishi, ili kunusuru kutokea kwa maradhi mbalimbali ya mripuko.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kisiwani humo Mratibu wa Kanda wa klabu hiyo Zanzibar Ali Juma Ali, alisema usafi wa mazingira ni moja kati ya njia inayoweza kuondosha maradhi ya mripuko yakiwemo ya kuharisha na kipindupindu, ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Alisema ni vyema usafi wa mazingira wanaoufanywa katika skuli zao wauendeleze katika maeneo yao yaliyowazunguka, ili kuweza kwenda sambamba na lengo la klub hiyo la utunzaji wa mazingira na kuleta afya njema kwa wanyama na jamii kwa ujumla.

Alisema maradhi ya mripuko yanahitaji kukingwa kwa kufanya usafi maeneo yote yakiwemo ya majumbani, kama wanavyofanya maskulini  kwa lengo la kujikinga na kujiweka salama kiafya.

Alifahamisha kuwa muonekano mzuri wa maeneo ya skuli yanayofanyiwa usafi wa mazingira yanapendeza, hivyo ni vyema kuhakikisha katika maeneo yaliyowazunguka yawe hivyohivyo.

Alielekeza kuwa wanafunzi hao wana jukumu kubwa la kutowa elimu ya usafi wa mazingira kwa jamii zao, ili kila mmoja aweze kujuwa thamani ya usafi wa mazingira na athari ya kupata maradhi mbalimbali ya mripuko.

“usafi wa mazingira ni moja kati ya jambo ambalo likiendelezwa, kufanywa katika sehemu tunazoendesha maisha yetu  maradhi ya mripuko yatakuwa ndoto tu kutokea”,alisema.

Kwa upande wake mratibu wa Mkoa wa Mjini Unguja Ame Haji Vuai, aliwataka walimu na wanafunzi hao kuwa wabunifu katika kutekeleza harakati za uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Alisema ni vyema kuidumisha klabu hiyo, ambayo kutekelezwa kwake itaweza kuokowa maisha ya wananchi ,mazingira na hata wanyama, hivyo ni vyema kuendelezwa kwa juhudi kubwa.

Nae Mratibu wa klabu Pemba Matti Ali Matti, alisema klabu hiyo ni ya hiari na imekuwa na uhuru wa kufanya shughuli za usafi wa mazingira, ili kila mmoja aweze kufanikiwa.

Alisema ni vyema kuipenda na kufanya kazi zinazohimizwa na klabu hiyo, ili kuweza kuondokana na matatizo ya kimazingira yanayoweza kuwapata binadamu na wanyama.

Mratibu wa vijana Lela Omar Abdi, alisema wana klabu hiyo wote wana lengo moja la kusaidia nchi na dunia nzima kuwa salama, katika maisha yao na kuwataka wanafunzi hao kufanya shughuli hizo kwa mahaba na mapenzi na kuleta faida.

Aliwafahamisha walimu na wanafunzi wanaoshughulikia klabu hiyo wasibweteke wanapokuwa na changamoto, badala yake waifikishe kwa viongozi wa klabu, ili kuweza kutatuliwa panapowezekana.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wanaosimamia klabu hiyo, mwalimu Mkubwa Ali Yussuf skuli ya Makoongwe alisema ni vyema walezi wa klabu hiyo, kupatiwa mafunzo mbalimbali ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira, ili waweze kuwa wabunifu zaidi.

Alisema wana klabu hiyo wasiangalie kutunza bustani pekee, badala yake wajikite na katika upandaji wa miti ya baharini na hata nchi kavu, ili kuweza kurejesha uasili.

“angalia kama sisi katika skuli yetu ya Makoongwe tunaendelea na shughuli za kutunza Popo na kutunza mikandaa jambo ambalo linasaidia sana katika nchi yetu”alisema.

Hivyo waliomba kuwepo kwa mashirikiano katika utendaji wa kazi zao za utunzaji na uhifadhi wa mazingira ambapo kufanikiwa kwake kunasaidia kuimarisha hali nzuri na kuondokana na madhila mbalimbali katika nchi kupitia mazingira, wanyama na jamii yote.