Thursday, January 16

Hafla ya ufungaji wa mafunzo ya ndoa mkupuo wa kumi yafanyika katika Msikiti wa Jaamiu Zinjibari

Baadhi ya Washiriki waliohitimu mafunzo ya ndoa wakiwa katika Ufungaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Kiembe Samaki Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katibu wa Mufti Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume akiwasisitiza Washiriki waliyohitimu  Mafunzo ya Ndoa kuitumia elimu walioipata  katika Ufungaji wa mafunzo hayo  huko  Msikiti wa Jaamiu Zinjibar uliopo Kiembe Samaki Mjini Zanzibar .

Baadhi ya Washiriki waliohitimu mafunzo ya ndoa wakiwa katika Ufungaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Kiembe Samaki Mkoa wa Mjini Magharibi.

Muhitimu wa Mafunzo ya Ndoa Msanif Mohamed Msanif akitoa neno la shukurani kwa Viongozi waliyowezesha mafunzo hayo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya ndoa huko  Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Kiembe Samaki Mkoa wa Mjini Magharibi.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Abdalla Hussein Kombo akimkabidhi Cheti cha Mafunzo ya ndoa Abdalla Khamis katika hafla ya Ufungaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Kiembe Samaki Wilaya ya Magharib ‘B’.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Abdalla Hussein Kombo akimkabidhi Zawadi Shekh Thabit Noman Jongo kutoka kwa Wanafunzi waliohitimu mafunzo ya ndoa mkupuo wa kumi hafla iliyofanyika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar uliopo Kiembe Samaki Mjini Zanzibar.

 

Picha Na Maryam Kidiko- Maelezo Zanzibar.

Na Khadija Khamis – Maelezo. 

Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi  Mheshimiwa Abdalla Husein Kombo amewataka wahitimu wa mafunzo ya ndoa kuitumia elimu hiyo kwa kujenga subira na uvumilivu ili kudumisha ndoa zao .

Hayo ameyasema katika Ukumbi wa  Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Mazizini wakati akikabidhi vyeti kwa Wahitimu wa Mkupuo wa kumi wa mafunzo ya ndoa.

Alisema lengo la kupatiwa mafunzo hayo kwa wanandoa ni kuwa walimu kwa wengine na kujenga imani subira na uvumilivu katika ndoa zao .

“Dawa pekee ya kudumisha ndoa ni kuwa na subira hasa kwa wanaume ingawa changamoto kubwa ni akinamama kukosa uvumilivu katika ndoa”alisema Waziri Kombo.

Aidha alisema katika dini ya kiislamu imetoa miongozo mbali mbali ya kisheria kwa lengo ya kuitunza ndoa na kuipa hadhi na  heshima yake kwa kubainisha haki na wajibu kwa wanandoa.

Nae Katibu wa Mufti  Shekhe Khalid Ali Mfaume amesema ameridhishwa na muamko wa wanafunzi wanaohitaji elimu ya ndoa jambo ambalo litasaidia kuepusha wimbi la talaka nchini.

Amesema mafunzo mbalimbali waliyoyapata wahitimu hao ni pamoja na maana ya ndoa kisheria, uchaguzi wa mchumba katika uislamu nafasi ya wazazi kwa wanandoa pamoja na sifa za familia ya kiislamu .

Alifahamisha kuwa licha ya mafunzo hayo wahitimu hao amefahamishwa viashiria vya migogoro katika ndoa na matokeo ya migogoro hiyo.

Nao wahitimu hao wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mufti  kwa kuwapatia mafunzo hayo bila ya malipo.

Walisema kuwa wataitumia elimu hiyo waliyoipata kwa vitendo kwa kujenga amani upendo na utulivu ili kudumisha ndoa zao na kupata familia bora.

Mafunzo hayo ni ya Mkupuo wa kumi yalifanyika kwa wiki kumi na kujumuisha Jumla ya Wanafunzi 195 Wakike na Wakiume .