Thursday, January 16

“Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni” …. “Mwisho wa kilio hichi ni lini?” Baba ambaka mtoto wa mkewe.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 

“INANIUMA sana sana, kwa sababu mdogo wangu ananiona mchungu kwa kule kumripoti mumewe Polisi baada ya kumbaka mwanawe aliemzaa kwa mume mwengine”, anasema mama mmoja mkaazi wa Msuka Wilaya ya Micheweni Pemba.

 

Ni mama mwenye umri wa miaka 45 alieamua kuifikisha kituo cha Polisi kesi ya mtoto wa ndugu yake baada ya kufanyiwa ubakaji na baba yake wa kambo.

 

Mwandishi wa makala haya aliamua kitega sikio kwa mama huyo, ili kujua hasa kilichomsibu mtoto huyo mwenye miaka 15 mkaazi wa Mtambwe Kaskazini Wilaya ya Wete.

 

Mama mkubwa wa mtoto huyo alnahadithia kwa uchungu kwamba, shemegi yake huyo amekuwa akimbaka mtoto huyo huku akimtishia kumchoma kisu iwapo atasema.

 

Anahadithia kuwa, baadhi ya siku mdogo wake huumwa na ugonjwa wa akili na huwa ana kawaida ya kwenda kumchukua na kuishi nae nyumbani kwake Msuka hadi pale atakapopona.

 

“Kipindi cha nyuma aliumwa, ndipo nilipomchukua nyumbani huku watoto wake wawili akiwaacha kwa baba yao wa kambo, alikaa zaidi ya wiki mbili”, anaeleza.

 

Siku moja akiwa kwenye pirika zake, ghafla alipokea simu kutoka kwa shemegi yake na kumtaka ampelekee mke wake na ndipo alipomchukua na kumpeleka kwa mumewe, ingawa tayari alikuwa ameshapata nafuu.

 

“Yule mdogo wangu alijaaliwa kupata ujauzito na alipotaka kujifungua aniliambia nikamchukue, nilikwenda na ndipo mwanawe wa miaka 15 akaniambia nimchukue hataki kuishi pale”, anahadithia mama huyo.

 

Dada huyo alifanya wasiwasi kiasi ambacho aliamua kumuuliza mtoto huyo na kumueleza kuwa, anapoondoka mama yake, baba yake wa kambo huingia chumbani mwao na kumbaka.

 

“Chango zilinisokota tumboni, kwa sababu nakumbuka shemegi yangu alivyonambia nimpelekee mke wake, kama sikumpeleka si angampa mimba mtoto huyu”, kwa kweli inauma.

 

Alimchukua mtoto huyo na mama yake na baada ya kufika nyumbani kwake alimuuliza maswali zaidi, ili ajue muda ambao ameshamfanyia kitendo hicho.

 

Baada ya mtoto kumuhadithia mama yake mkuu anagundua kuwa, kumbe alikuwa anamfanya kama mke wake hata ikiwa mama yake yupo na kuhtishia kisu ili asime.

 

“Hali hiyo ilimchosha mtoto huyo na kuona bora avunje ukimya na kuamua kuniambia mimi, hivyo nitahakikisha mwanangu anapata haki yake”, anaelezea.

 

Ndipo alipochukua hatua ya kwenda kuripoti kesi hiyo kituo cha Polisi na ndipo walipoanza kuhasimiana mdogo wake kutokana na hatua aliyoichukua kwamba hakuridhika nayo.

 

“Mdogo wangu ananiona adui yake kwa sababu nilikwenda kumshitaki mumewe, kwa hivyo anashirikiana na mkwe wake, ili mumewe aachiwe huru”, anaelezea.

 

Kinachomuumiza kwa sasa, ni kumuona mdogo wake anadhalilika, kunyanyaswa na kutukanwa na mkwe wake kwa sababu ya kuwekwa mwanawe rumande.

Mama huyo anasema, kila siku anamwambia arudi zake ili asiteseke ingawa anachakugua kuteseka kutokana na kumpenda mumewe ambae hamtakii mema, kwani asingelimbaka mwanawe.

 

“Mkwe wake aliwahi kuniambia kuwa, watoto wake watatu walibakwa lakini alinyamaza mpaka wakaolewa, kwanini mimi sikunyamaza”, anahadithia.

 

Ingawa yeye hakuyasikiliza maneno hayo na alichukua jititihada ya kulifikisha kwenye vyombo vya sheria, ili pia kuikomesha jamii yenye tabia ya kunyamaza wakati mtoto anapodhalilishwa.

 

Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho anaeleza kuwa, baba yake alikuwa anamtishia kumchoma kisu na ndio maana alikuwa hamwambii mama yake.

 

“Baba alikuwa anakuja chumbani kwetu kila siku usiku na kunibaka, nalala na ndugu zangu lakini ananifanyia kitendo hicho cha ukatili”, anafafanua.

 

Kilichokuwa kinamuumiza ni kuona kuwa, baba yake huyo ana mwanawe mzazi ambae wanalala pamoja ingawa hamfanyii kitendo hicho.

 

“Nilipochoka ukatili ule aliokuwa akinifanyia baba yangu wa kambo, nilimuhadithia mama yangu mkubwa”, anahadithia mtoto huyo.

 

Ndugu wa mama mmoja na mtoto huyo anaeleza, alishawahi kumuona baba yake usiku mkubwa akiwa kwenye chumba chao, ingawa hakujua anataka kitu gani.

 

“Nilimuona baba anaingia chumbani tunacholala, lakini sikujua anataka nini, nilifikiri anatafuta kitu, kwa iyo sijui kitu ambacho alitaka kufanya”, anaelezea.

 

Shufaa Asaa Muombwa ambae ni sheha wa Shehia ya Mtambwe Kaskazini anaeleza kuwa, kesi hiyo tayari imeshafikishwa mahakamani inaendelea kusikilizwa mashahidi.

 

“Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata baada ya kufanya uchunguzi, huyo mtoto alifanyiwa kitendo hicho tangu mwaka 2019, ingawa wazazi wake walificha mpaka wamesema mwaka huu”, anasema sheha huyo.

 

Kinachomshangaza ni kuona kuwa tangu mwaka 2019 alipobakwa mtoto huyo familia ilificha na kusema mwaka huu, jambo ambalo linamfanya atafakari kila wakati kitu kilichosababisha.

 

“Itakuwa hapa kuna kitu kimejificha, kwa nini hawakusema hizo siku za nyuma na wamesema saivi? wakati mtoto ameshaharibiwa sana, kwa kweli jamii tunahitaji kubadilika”, anbaeleza.

 

Anasema kuwa, bado jamii inagubikwa na rushwa muhali, hali ambayo inasababisha ongezeko la kesi za udhalilishaji siku hadi siku.

 

Sheha huyo anasema, ipo haja kwa Serikali na taasisi binafsi kuchukua juhudi ya kuwaelimisha wanajamii, ili wajue madhara ya rushwa.

 

“Rushwa ina uwanja mpana kwenye kesi hizi, jamii huwa na rushwa muhali na hata rushwa ya pesa, kwa sababu wazazi wengine huchukua pesa kutoka kwa mtuhumiwa, ili kesi isiende mbele”, anaeleza.

 

Tatu Abdalla Mselemu ambae ni Mratibu wa Jumuiya ya TUJIPE Pemba anasema, wamekuwa wakichukua juhudi ya kuielemisha jamii juu ya kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto, ingawa bado nguvu zaidi zinahitajika.

 

Anafahamisha kuwa, kuibadilisha jamii kutoka jambo fulani hadi kufikia unalotaka, kunahitajika muda na nguvu za pamoja kuhakikisha wanaondosha kabisa vitendo hivyo.

 

“Tunajitahidi kuwaelimisha na kuwafahamisha kwamba, janga hili sio la kufumbiwa macho, watoto ni wetu, usimuone mtoto wa mwenzako amefanyiwa udhalilishaji ukaona na wako atasalimika, tupige vita ili watoto wote wawe salama”, anafahamisha.

 

Mratibu wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC) Mgeni Kombo Khamis anasema kuwa, katika kuunga mkono mapambano dhidi ya udhalilishaji, wamekuwa wakitoa waandishi kwenye klabu hiyo kuwapeleka kwenye mafunzo ya Udhalilishaji Tanzania bara.

 

“Tulikuwa kila mwaka tunapeleka waandishi wawili kwa mafunzo ya GBV, inagwa tangu nchi ilipokumbwa na janga la Corona hatujawafanyia mafunzo hayo”, anaselezea.

 

Anasema, lengo lao ni kuwaongezea ujuzi, ili wafanye kazi zao kwa ufanisi, sambamba na kuijenga jamii kufahamu madhara ya udhalilishaji na kuachana na dhana ya kuoneana muhali.

 

“Asilimia kubwa ya matukio haya yanatokea ndani ya familia zao na ndio maana wanakuwa wagumu kuripoti, sasa tunaamini kwa mafunzo haya wanayoyapata wanahabari itasaidia sana kuijenga jamii iliyobora”, anafahamisha.

 

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kaskazini Pemba Fakih Mohamed Yussuf anaeleza, kesi hiyo ilifikishwa kituo cha Polisi Wete, ambapo zilifanyika taratibu za kiupelelezi na baada ya kumaliza ikafikishwa mahakamani.

 

“Uchunguzi wa haraka ulifanyika na kesi hiyo kufikishwa mahakamani, baadhi ya mashahidi wameshasikilizwa na kwa sasa inaendelea”, anafahamisha Mkuu huyo.

 

Fat-hiya Mussa Said anaeleza kuwa, kuna msemo usemao…. ‘umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu’, hivyo ushirikiano unahitajika zaidi kupambana na janga hilo ambalo huwakosesha furaha watoto.

 

“Tusichoke kupambana licha ya changamoto tunazokumbana nazo, tuwe na moyo wa kujitolea ili kuona kwamba vitendo hivyo vinaondoka kabisa katika jamii yetu”, anasema mratibu.

 

Anafafanua kuwa, kuna njia mbali mbali ambazo wanazitumia katika kuhakikisha jamii inaondokana na muhali na inakuwa mstari wa mbele kutoa ushahidi.

 

“Ushahidi ndio jambo muhimu ambao ndio unaoweza kumtia hatiani mtendaji wa kosa, hivyo nguvu zetu tumezielekeza huko kwa kuwajengea uwezo wahanga na wazazi wao, ili kuona litasaidia vipi mapambano hayo”, anaeleza.

 

Akizungumzia kesi hiyo anasema, wamekuwa wakiwaita na kuwajengea uwezo katika suala zima la kwenda kutoa ushahidi mahakamani, ili kuona kuwa haki inatendeka.

 

Kwa mujibu wa Sheria, kumuingilia maharimu ni kosa kinyume na kifungu cha 143 (1) (2) (4), cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 ambapo kifungu kidogo cha (1) na (4) kinaeleza kwamba ni kosa kumuingilia maharimu wako na ukipatikana na kosa mshitakiwa atahukumiwa kwenda chuo cha mafunzo maisha au miaka 25.