Thursday, January 16

ZFDA yapendekeza bidhaa kufanyiwa tena uchuguzi zinapoingizwa kisiwani Pemba.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAKALA wa Chakula na Dawa (ZFDA) Pemba imependekeza kufanyiwa uchunguzi kwa mara ya pili bidhaa zinapofika kisiwani Pemba, ili kuepusha kuharibika ama kufanya udanganyifu.
Akizungunza na mwandishi wa habari hizi baada ya kuzuiwa mchele polo 400 aina ya Sunflower Rice kwenye meli ya sea star 1 Julai 10 kutoka Unguja, Mkurugezi wa ZFDA Pemba Nassir Salum Buheti alisema, ni vyema bidhaa zinapofika Pemba zifanyiwe tena uchunguzi wa mara ya pili.
Alisema kuwa, bidhaa nyingi huharibika ghalani ama kufanyika udanganyifu wa kuweka bidhaa mbovu kwenye vifungashio vipya, hivyo ipo haja ya kufanya uchunguzi kwa mara ya pili na kuchukuliwa sampuli kila baada ya miezi mitatu (Post marketing surveillance), ili kuepuka udanganyifu.
“Wafanyabishara wanafanya udanganyifu na kuwalisha wananchi vyakula vibovu, hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha yao, hivyo tunapendekeza kufanyiwa uchunguzi wa mara ya pili bidhaa zinazoingia Pemba hasa za mchele, hii itasaidia kulinda afya ya mlaji”, alisema Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia suala la mchele ulifika bandari ya Wete Julai 10 mwaka huu, ni polo 400 zenye ujazo wa kilogramu 50 kwa kila moja, ambao ni mali ya wafanyabiashara Abdi Abdalla na Saleh Mbarouk Kombo, ambapo baada ya kupelekwa maabara uligundulika kwamba haufai kwa matumizi.
Alieleza kuwa, baada ya kupata majibu hayo, Wakala wa chakula makao makuu iliamua kwenda kuchukua sampuli nyengine ya mchele huo Ghalani mwa muingizaji kwa ajili ya uchunguzi na kubainika kuwa haufai kwa matumizi.
Mkurugezi huyo alieleza kuwa, baada ya kuona kwamba mchele huo usiofaa kwa matumizi ushaingizwa sokoni, walitengeneza timu ya ukaguzi kwa ajili ya kuhakikisha unazuiliwa usitumike, ambapo walifanikiwa kuzuia polo 1,018 katika maeneo mbali mbali kisiwani Pemba na kupanga utaratibu wa uteketezaji.