NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WANAWAKE waliogombea mwaka 2020 wamesema, ili kuhakikisha wanafikia 50-50 kwenye vyombo vya kutoa maamuzi ni vyema wakashirikiana pamoja kuanzia ngazi ya Jimbo hadi kwenye jamii.
Wakizungumza katika mkutano wa tathmini baada ya kumaliza uchaguzi mkuu mwaka 2020 uliofanyika katika Ukumbi wa Jamhuri Wete walisema, wanawake hukosa mashirikiano kuanzia kwenye ofisi zao za Jimbo, jambo ambalo linawarudisha nyuma.
Walisema kuwa, kumekuwa na fitina za chini kwa chini kwamba mwanamke hafai kuwa kiongozi na hatimae kuwashawishi wajumbe wasimpe kura, jambo ambalo linawavunja moyo katika harakati hizo za kugombea nafasi za uongozi.
“Kwa kweli shida inaanzia kwenye ofisi za majimbo yetu, wale viongozi huwashawishi wajumbe wasimpe kura mwanamke, wanasema hatuwezi lolote kazi yetu ni kupika tu”, walisema wagombea hao.
Waleleza kuwa, ipo haja kwa viongozi wa majimbo kupewa elimu, ili wachague mtu kwa utendaji wake na sio kwa kuwa anahulikana sana, kwani hawatofikia lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“Mimi ni mtendaji mzuri sana na utendaji wangu unaonekana kila mahala, lakini nilipoamua kugombea niliambiwa wewe mwanamke nenda kazae tu, wanaosema hivyo ni viongozi wetu”, alisema mgombea Asha Omar Said.
Kwa upande wake mgombea Riziki Abdalla Omar alieleza kuwa, wamekuwa wakijitahidi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kugombea uongozi ingawa fitina za viongozi wao ndio zinazowaumiza.
“Wanawake tunajiamini na tunasimama imara kutetea haki yetu lakini kwa hali tunayofanyiwa na viongozi wetu, maisha hatutofika mbele maana wao ndio wanaohamasisha wajumbe tusipigiwe kura”, alieleza.
Nae mgombea Faida Juma alisema kuwa, kitu chengine kinachowavunja moyo ni kuona kwamba wanawake wenzao ndio ambao wanawadharau na kuwakebehi na hatimae kuwawekea chuki zisizo na msingi.
Amira kutoka Jimbo la Gando Salma Khamis Juma alieleza kuwa, kutambulika ni jambo muhimu sana, hivyo kuanzia sasa wanawake wachukue jitihada za kuwa karibu na jamii, ili watakapogombea uongozi iwe tayari imeshawakubali.
“Wanawake ni watu wa huruma, tuna imani, hivyo tutakapoingia kwenye vyombo vya kutoa maamuzi tutaisaidia jamii kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili”, alisema.
Amira kutoka Jimbo la Wete Asya Amour Abrahman alisema, pamoja na changamoto zilizowakabili katika chaguzi zilizopita, sasa ni wakati wa kujipanga upya, ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 wanaingia majimboni kuusaka uongozi.
“Tumtegemee Mungu katika mambo yetu, yeye ndie mwenye uwezo wa kukupa, hivyo tusikate tamaa, kipindi kilichopita haikuwa riziki yetu sasa tujiandae kwa baadae”, alisema Ukhti huyo.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said alisema, ili chaguzi zijazo wajitokeze kwa wingi kugombea uongozi, Kuna haja ya kukaa pamoja na kuandaa mikakati ambayo itawasaidia.
Mkutano huo ambao umewashirikisha viongozi wanawake waliofanikiwa na ambao waliogombea na hawakufanikiwa, ulikuwa na lengo la kujitathmini baada ya kumaliza uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.