Monday, November 25

Wadau wa Kupambana na dawa za Kulevya Zanzibar wakutana.

NA ABDI SULEIMAN.

Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar imesema itayafanyia kazi maoni yoe yaliyotolewa na wadau mbali mbali, juu ya sheria ya kupambana na dawa za kulevya Zanzibar, ili kuweza kupata sheria iliyo bora zaidi ya kukabiliana na madawa ya kulevya nchini.

Aidha Tume hiyo imesema itaendelea kukusanya maoni, ili kuona wadau wanasema nini, katika kuboresha rasimu hiyo ya sheria kabla ya kupelekwa barazani kujadiliwa na kuwa sheria kamili.

Akizungumza katika mkutano wa Wadau sheria ya Kupambana na dawa za Kulevya Zanzibar, ukiofanyika katika ukumbi wa Ofis ya Rais Katiba, sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali pamoja na kamati za ulinzi na usalama Pemba.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Khadija Shamte Mzee, alisema sheria hiyo imekuwa na changamoto mbali mbali, hali inayopeleka kukwamisha jitihada za kupambana na dawa za kulevya nchini, hivyo ipo haja ya kuunganisha nguvu za pamoja kwa viongozi, ili kufikia lengo katika vita hivyo.

“Tumeshapita sehemu mbali mbali katika kukusanya maoni, ili tuweze kutengeneza sheria bora na imara itakayoweza kuipa Mamlaka kamili tume yetu, tena kusiwe na mvutano katika ukamataji wa dawa za kulevya”alisema.

Alisema baada ya kukamilika kazi ya kukusanya maoni tutaweza kupeleka mswada serikali, iweze kupitishwa na kuwa mamlaka kamili uweze kufanya kazi zake.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud, aliitaka tume ya kurekebisha sheria kufika kwa watu wengi katika ukusanyaji wa maoni yao, ili kutengeneza sheria itakayokuwa bora katika kupambana na dawa za kulevya.

Alisema dawa za kulevya ni hatari sana, zimekuwa zikiathiri vijana kwa kiasi kikubwa, vita hivyo ni kupambana na watu wakubwa, lazima sheria hii itakapotoka iwe kali sana kama ilivyo kwa nchi za wenzetu.

“Sote tupo hapa katika kutoa maoni yetu ambayo yatatumika katika utengenezaji wa sheria ya kupambana na dawa za kulevya, sipendi kumuona mtu ananipigia simu kama aliyekamatwa ni jamaa yake, lazima tuwe wakweli katika hili, ikiwa hili janga halijakufika wewe kila kitu utaona sawa”alisema.

Aidha alifahamisha kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha dawa za kulevya haziingii nchini, huku akiitaka jamii kusaidia katika mapambano ya kwa lengo la kuwa na taifa lenye vijana bora.

Naye Mkurugenzi Mtendaji tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar Kanali Burhani Zuberi Nasoro, alisema sheria ya dawa za kulevya imetungwa zamani na imeshafanyiwa marekebisho mengi ndio maana wanatengeneza sheria mpya itakayoipa tume mamlaka kamili.

Alisema maboreshaji hayo ya sheria yataweza kukinusuru kizazi kilichopo, kwani zipo nchi wametengeneza sheria kali sana ambazo dawa za kulevya ngumu kuingia nchini humo.

Katibu wa Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar Mussa Kombo Bakar, alsiema sheria inagusa watu wengi lazima kukutana na makundi mbali mbali ili tuweze kuwa na sheria iliyobora zaidi.

Wakitoa maoni yao wadau hao wamesema mtu yoyote atakaekamatwa kuhukumiwa kifungo cha maisha, sambamba na kuwepo kwa chombo maalumu kitakachoweza kupeleleza mwenendo wakesi inavyokwenda pamoja na utoaji wake wa hukumu yake.

Walisema ukiondosha udhaifa wa baadhi ya wasimamizi wa sheria ya madawa ya kulivya, bado baadhi ya vifingu vya sheria vimekuwa havikidhi mahitaji ya sheria hizo.