Sunday, October 20

Wabunge wapya wasaidia vifaa hospital ya Wete.

MBUNGE wa Jimbo la Gando Salum Mussa Omar na Mbunge wa Jimbo la Kojani Hamad Hassan Chande (katikati), wakimkabidhi Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wete Dk.Khamsi Rashid Salum, vifaa mbali mbali kwa ajili ya hospiatli hiyo, vikiwemo mafeni, Box za Taizi, Glavu na kiti cha kubebea wagonjwa.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

MBUNGE wa Jimbo la Gando Salum Mussa Omar na Mbunge wa Jimbo la Kojana Hamad Hassan Chande, wamekabidhi vifaa mbali mbali pamoja na Fedha taslimu shilingi Milioni 1.2, kwa uongozi wa Hospitali ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa na wabunge hao, ni pamoja na mafeni, boks za Taizi, Glavu na dawa za usafi na kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa AIC.

Makabidhiano hayo yaliofanyika katika hospitali hiyo Wete, ikishuhudiwa na watendaji mbali mbali wa Hospitali na baadhi ya wananchi waliofika hospitalini hapo kuwaona jamaa zao.

Akizungumza katika hafla hiyo, mbunge wa Jimbo la Gando Salumu Mussa Omar alisema licha ya kukabidhi vifaa hivyo, lakini haridhishwi na hali ya mazingira ya hospitali hiyo ilivyo, pamoja na kutokufanya kazi kwa baadhi ya mashine muhimu za vitengo vya hospitali hiyo.

Alisema kutokufanya kazi kwa mashine ya X-Ray na Ultra Sound ni kurudisha nyuma maendeleo ya Hospitali hiyo, pamoja na kuwazidishia usumbufu wananchi wa Wilaya ya Wete kufuata huduma hizo, katika hospitali ya Wilaya ya Micheweni au Chake Chake.

Alisema katika Mwezi Mmoja hospitali hiyo, inapokea wagonjwa 300 hadi 600 wanaohitaji huduma ya X-Ray, kwa sasa wagonjwa wanalazimika kufuata huduma hizo wilaya nyengine.

“Kwa hali hii hatuwezi kufikia maendeleo hata kidogo, hospitali kama hii kubwa leo inakosa vitu muhimu kama hivyo, hebu tizama hapa gari ya kubebea wagonjwa zipo mbili, lakini unaambiwa moja ndio inayofanya kazi moja haifanyi, hili ni jambo la kusikitisha kwa hospitali kama hii”alisema.

Aidha Mbunge huyo alimtaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa habaraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, kuiangalia hospitali hiyo kwa jicho la tatu, ili wananchi waweze kupata huduma bora za matibabu.

Mbunge huyo alisema wafanyakazi wa hospitali hiyo wamejawa na woga wa kusema, hata changamoto zao kwa viongozi wanaofika hispitalini hapo, wakihofia kuondoshwa au kuhamishiwa sehemu nyengine iwapo watasema madhila yaliyopo hospitalini hapo.

“Kama itakuwa kila siku tunaenda kwa mtindo huu, basi hata Dk.Mwinyi atakuwa anadanganywa, wakati serikali yake imedhamiria kuleta mabadiliko katika maeneo yote”alisema.

Naye mbunge wa jimbo la Kojani Hamada Hassan Chande, alisema lengo la ziara yao ni kukabidhi vifaa, lakini walisikitishwa na hali halisi ya hospitali hiyo ilivyo baada ya kuwananchi kudai baadhi ya vifaa havifanyi kazi.

Alisema kutokufanya kazi kwa baadhi ya vifaa muhimu katika hospitali, hiyo ni kurudisha nyuma maendeleo ya sekta ya afya, huku wakimuomba makamu wa Pili wa Rais kufanya ziara katika hospitali hiyo.

“Hili ni jambo la kusikitisha kuona mashine muhimu hazifanyi kazi, hii sio sehemu ya kufanyia masihara sehemu hii wananchi wanahitaji kuokoa maisha yao mashine muhimu hazipo”alisema.

Hata hivyo aliwataka viongozi wenzake wa majimbo, kuitupia jicho la huruma hospitali hiyo, kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wananchi wa kwenda wilaya ya chake chake au wete kufuata matibabu.

Naye Daktari dhamana wa hospitali ya Wete, Dk.Khamis Rashid Salum, alisema vifaa walivyokabidhiwa watavitumia kwa lengo lililokusudiwa, kwani vifaa hivyo vimefika kwa wakati muwafaka.

Alisema changamoto kubwa kwa sasa inayowakabili, ni pamoja na uwepo wa majengo yapo hali mbaya kwa sasa, kuharibika kwa X-Ray, mashine ya kupimia wagonjwa wa ini, mafigo, Ultra Sound ambapo huduma hizo kwa sasa mgonjwa hulazimika kuzifata Hapitali ya Wilaya ya Micheweni au Chake Chake.

Alisema tatizo mashine ya kuchomea takataka za hospitali kwa sasa haifai, licha ya kufanyiwa ukarabati inastahili kujengwa nyengine, ambapo ukarabati hazipunguwi Milioni 14 wakati mpya kujengwa ni milioni 20.

Kwa upande wake daktari wa masuala ya Usingizi na ganzi katika chumba cha operesheni Ali Othaman Ali, alisema huwezi kuwa na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), bila ya kuwa na Oxygen ya kutosha.

Naye Mkuu wa kitengo cha lishe Pemba Raya Mkoko Hassan, amesema anasikitishwa sana na baadhi ya wafanyakazi kushindwa kuyaeleza matatizo yanayowakabili, katika utendaji wao wa kazi hali inayowafanya wafanye kazi katika mazingira magumu.

Alisema suala la chakula kwa hospitali zote za Pemba, imekuwa ni tatizo katika utekelezaji wake baada ya kuwasilisha taarifa ofisi kuu ya wizara ya afya.

MBUNGE wa Jimbo la Gando Salum Mussa Omar na Mbunge wa Jimbo la Kojani Hamad Hassan Chande (katikati), wakimkabidhi Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wete Dk.Khamsi Rashid Salum, fedha taslimu shilingi Milioni 1.2 kwa ajili ya ununuzi wa AIC kwenye chumba cha huduma ya mama na mtoto.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)