Friday, January 17

UFAFANUZI WA MADARAJA MATATU YA ZFF NA IDADI YA TIMU ZAKE PAMOJA ZILIVYOPATIKANA TIMU

Msimu mpya wa Soka la Zanzibar wa Mwaka 2021-2022 kutakua na Ligi 3 kubwa zitakazosimamiwa na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF).
1. Ligi Kuu Soka ya Zanzibar (ZPL) itakuwa na timu 16 ambazo ni Timu 10 zilizobakia kwenye msimu uliopita ambazo ni KMKM (Mabingwa Watetezi), Zimamoto,KVZ, Mafunzo, JKU, Kipanga, Malindi, Mlandege, Polisi na Black Sailors, kisha zitaungana na timu 2 za juu kutoka Daraja la Kwanza Taifa Unguja ambazo ni Uhamiaji na Taifa ya Jang’ombe, hapo zitakuwa 12, utajumlisha timu 4 kutoka Daraja la Kwanza Pemba, ukipiga hesabu zitakuwa zimetimia jumla ya timu 16, yani 2 zimepanda kutoka Unguja na 4 kutoka Pemba.
2. Ligi ya Taifa Zanzibar (Zanzibar National league (ZNL) daraja hili litakuwa na timu 12 Unguja na 12 Pemba kwa kuanzia litaanza kuchezwa kwa mfumo huo wa Kikanda lakini lengo lake liwe daraja 1 tu la ZNL yani Ligi iwe ya Zanzibar kwa ujumla na sio mfumo wa Kikanda.
Jinsi ya kupatikana hizo timu, mfano kwa Unguja ni zile timu 8 zilizobakia kwenye Ligi ya Daraja la Kwanza Unguja msimu uliopita ambazo ni Kilimani City, Mchangani Fc, Ngome, Dulla Boys, Mwembe Makumbi, New King, Jang’ombe Boys na Gulioni Fc, hizo zitakuwa 8 jumlisha na 1 timu ya Chuoni iliyoshuka kutoka Ligi Kuu, hapo zitakuwa 9, jumlisha na timu 3 kutoka kwenye Mikoa yani Kila Bingwa wa Mkoa atapanda hapo kwaiyo kwa Mikoa 3 ya Unguja itakuwa timu 3 hizo, kwa Maana ya Mkoa wa Kusini Unguja timu 1, Mkoa wa Kaskazini Unguja timu 1 na Mkoa wa Mjini Magharibi timu 1, ukipiga hesabu hapo ni timu 12 hizo ndo zitacheza ZNL kwa Unguja na Pemba itakuwa kama hivyo nako huko 12.
3. Ligi daraja la kwanza kanda. Daraja hilo litakuwa na timu 14 Unguja na 14 Pemba, jinsi ya kupatikana timu hizo kwa Unguja itakuwa timu 2 zilizoshuka Daraja la Kwanza msimu ulopita ambazo ni Idumu na Mchangani United ambazo hizo hazitorudi Mkoani kwao zitacheza daraja hilo, swali litakuja kwaiyo zitacheza timu 2 tu pekee, hapana nyengine zitatoka Mikoani ambapo kila Mkoa utatoa timu 4, kwaiyo kuna mikoa 3 ya Unguja ukipiga hesabu zitakuwa timu 12 zimetoka Mikoani, yani Kusini Unguja 4, Kaskazini Unguja 4 na Mjini Magharibi 4, ukijumlisha na zile 2 Idumu na Mchangani United zitakuwa 14, hilo ndilo Daraja la Kwanza Kanda Unguja na Pemba itakuwa kama hivyo.
Ufafanuzi huo umetolewa na Mrajis (Msajili) wa Vyama vya Michezo Zanzibar Abubakar Mohammed Lunda na kuandikwa na Abubakar Khatib (Kisandu).