Sunday, October 20

MBUNGE wa jimbo la Gando kupitia CCM Salim Mussa Omar, aungana na wanachama wa jimbo hilo, katika usafi

BAADHI ya wananchi wa jimbo la Gando Wilaya ya Wete wakifanya usafi katika eneo ambalo linatarajiwa kujengwa Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo huko katika Kijiji cha Minyenyeni Wilaya ya Wete,( PICHA NA SAID ABDULRAHMAN PEMBA)

NA SAID ABRAHMAN.

 

MBUNGE wa jimbo la Gando kupitia CCM Salim Mussa Omar, ameungana na wanachama wa jimbo hilo, katika usafi wa eneo ambalo linatarajiwa kujengwa kwa Ofisi ya Mbunge wa jimbo.

 

Akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM, waliojitokeza katika usafi huo katika Kijiji cha Minyenyeni jimbo la Gando, alisema kuwa tayari bajeti ya jengo hilo imekamilika.

 

Alisema kuwa lengo la kujenga Ofisi hiyo ni kuwaondoshea adha wananchi wake, wakati wa kukutana nao ili waweze kumueleza shida zao zinazowakabili katika jimbo lao.

Salim alifahamisha kuwa wanajenga Ofisi hiyo, kwa mara ya kwanza tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama hapa nchini, hakuna Mbunge hata mmoja aliyethubutu kujenga Ofisi ya Mbunge ndani ya jimbo hilo.

 

“Tokea kuasisiwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini, sisi vijana tulikuwa tunapata shida sana kuonana na Mbunge wetu, ili tuweze kumueleza shida zetu, mara hii tumeamua kwa makusudi kuanzisha Ofisi yetu ya Mbunge, mwakilishi pamoja na Diwani Ofisi hiyo, itakuwa na ukumbi wa kisasa wa mikutano utakaochukua idadi ya watu 500 hadi 700 kwa wakati mmoja,” alisema Mbunge Salim.

 

Aidha alisema ujenzi wa ofisi hiyo hautozidi miezi minne, kukamilika kwake kwani wamejipanga vizuri kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati.

 

Mbunge Salim aliwataka wanachama hao kuacha tabia ya kufuata viongozi wao kwa mambo binafsi, badalayake kutoa fikra zao kwa viongozi wao zitakazoweza kuwaletea maendeleo katika jimbo lao.

Nae mwenyekiti wa jimbo la Gando Massoud Ismail Juma, alimpongeza Mbunge huyo kutokana na maamuzi yake ya busara ya kuamua kujenga Ofisi hiyo, ambayo itaweza kumfanya Mbunge au Mwakilishi kupatikana kwa urahisi na wakati wowote.

 

Aidha Massoud alifahamisha kuwa mbali na kupatikana kwa viongozi hao, lakini wanancha na wananchi kwa ujumla wataweza kulitumia jengo hilo kwa shughuli mbali mbali za mikutano.

 

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa jimbo hilo linataka kuweka historia kwa Zanzibar, kwa jinsi gani inavyotakiwa Mbunge au Mwakilishi awe baada ya kuingia madarakani.

 

“Hi ni ishara tosha kwa Mbunge wetu kuwa na imani na wananchi wake, katika awamu zote zilizopita hakuna Mbunge yeyote aliyethubutu kujenga Ofisi yake kwa malengo ya kusikiliza kero za wananchi, Ofisi zao zilikuwa chochoroni tu,” alisema Mwenyekiti huyo.

 

Nae Katibu wa CCM jimbo la Gando Asha Omar Rashid, alieleza kuwa endapo jengo hilo litamalizika wananchi watanufaika sana kwa kupeleka matatizo yao sehemu inayohusika na kupatiwa ufumbuzi wake.

 

Aidha alifahamisha kuwa Ofisi hiyo haitochagua ni mwanachama gani, ambae anastahiki kufika hapo na kusikilizwa shida bali itaweza kusaidia wananchi wote wa jimbo hilo.

 

Nae Riziki Abdalla Omar alisema kuwa wazo la kujengwa Ofisi ya Mbunge ni jambo zuri, kwani hapo awali hakuna hata Mbunge au Mwakilishi hata mmoja, aliwahi kujenga Ofisi ili kukaa pamoja na wananchi na kuwasikiliza kero zao.