Thursday, January 16

Ligi ya Premia: Fifa imewapiga marufuku wachezaji waliokataa kuziwakilisha Brazil, Mexico, Chile na Paraguay

Maelezo ya picha,Roberto Firmino wa Liverpool na Gabriel Jesus wa Manchester City ni miongoni mwa wachezaji wanane wa Brazil ambao watazuiwa kuchezea vilabu vyao wikendi hii

klabu za Ligi Kuu ya Premia zinatumai wachezaji wao watapatikana wikendi hii licha ya mataifa manne kuchochea sheria ya kuwazuia kucheza.

Wachezaji ambao hawakusafiri baada ya kuitwa na Brazil, Mexico, Paraguay na Chile wamepigwa marufuku kwa siku tano chini ya kanuni za Fifa.

Maafisa wanafanya mazungumzo na Fifa kujaribu kutafuta njia ya kutatua suala hilo.

Manchester City, Manchester United, Liverpool, Leeds, Chelsea, Wolves, Newcastle na Watford zimeathirika.

Wachezaji wanane kutoka vilabu vitano wameathiriwa na uamuzi wa Brazil peke yake, ambayo inafuata hatua sawa na Mexico, Paraguay na Chile iliyochukuliwa wiki iliyopita.

Brazil iliweka marufuku hiyo baada ya Ligi Kuu ya Premia kuwazuia wachezaji kuonekana kwa nchi zao ikiwa ilimaanisha kusafiri kwenda kwa nchi zilizo miongoni mwa orodha ya zile zilizopigwa marufuku kuingia.

Wachezaji wanaosafiri kwenda kwenye nchi zilizo katika orodha hiyo wangepaswa kukosa michezo kadhaa baada ya kurudi kwasababu ya kipindi cha siku 10 cha kujitenga kinachohitajika chini ya sheria za Uingereza kama njia moja ya kukabiliana na janga la corona.

Mbali na kukosa mechi za upande wao za wikendi, mlinzi wa Chelsea Thiago Silva na kiungo wa kati wa Manchester United Fred pia hawataruhusiwa kucheza katika michezo yao ya ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Zenit St Petersburg na Young Boys Jumanne.

Hata hivyo, inaeleweka kuwa Brazil haijaomba mshambuliaji wa Everton Richarlison azuiliwe katika mechi dhidi ya Burnley Jumatatu.

Hatua ambayo kuna wale wanaohisi Brazil ilionyesha huruma katika kesi hiyo kwani Everton ilimruhusu Richarlison kucheza kwenye Michezo ya Olimpiki wakati kanuni hazikuwa zinawalazimisha.

Hatua hiyo pia inaathiri wachezaji watatu wa Liverpool, Roberto Firmino, Fabinho na Alisson, wachezaji wawili wa Manchester City Ederson na Gabriel Jesus, na mshambuliaji wa Leeds Raphinha, ambaye alikuwa ameitwa kwenye kikosi cha Brazil kwa mara ya kwanza.

Wolves na mshambuliaji wa Mexico Raul Jimenez; kiungo wa kati wa Newcastle raia wa Paraguay Miguel Almiron na mlinzi wa Watford raia wa Chile Francisco Sierralta pia wameathiriwa.

Kufikia sasa, hakuna kati ya vilabu vilivyoathirika kimetoa taarifa yoyote kwa umma juu ya jambo hilo.

Hata hivyo, inajulikana kuwa wanahisi hali hiyo haizingatii hali zisizo za kawaida ambazo wamejikuta na wanahisi wachezaji wanapaswa kuruhusiwa kucheza kwa vilabu vyao wikendi hii.

Ligi Kuu ya Premia, FA, Serikali na Fifa zote zinadhaniwa kushiriki katika majadiliano.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ligi Kuu ya Uingereza Richard Masters pia ameandikia vilabu kusema anajaribu kupata suluhisho.

Inahisiwa kuwa mabadiliko yoyote katika hali hiyo yangehitaji aina fulani ya hakikisho kwamba wachezaji watapewa msamaha wakisafiri kipindi hiki cha kukabiliana na virusi vya corona ili waweze kutimiza majukumu yao ya kimataifa mnamo mwezi Oktoba na Novemba, ambayo rais wa Fifa Gianni Infantino amekuwa akisisitiza.

CHANZO CHA HABARI BBC