Monday, January 27

DIAMOND PLATINUMZ KUSHEREHESHA UZINDUZI WA UELIMISHAJI WA SENSA YA WATU NA MAKAZI JIJINI DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri.

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

MSANII maarufu nchini Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platinums kusherehesha tukio la uzinduzi wa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Akiongea na waandishi wa Habari ofisini kwake usiku huu, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema kuwa tukio hilo la kihistoria litafanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Shekimweri alisema “uzinduzi wa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 utafanyika kesho tarehe 14 Septemba, 2021 katika uwanja wa Jamhuri. Mgeni rasmi katika uzinduzi huo atakuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan”.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa tukio hilo litashereheshwa na wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya akiwepo Diamond Platnums anayetarajiwa kuwasiliki kesho asubuhi na kuingia uwanjani moja kwa moja. Wasanii wengine aliwataja kuwa ni Ben Paul, Bushoke na Moni Centrozone. “Kwenye taarifa ya awali mlijulishwa kuwa kutakiwa na vikundi vya burudani, ngoma, kwaya na wasanii wa kizazi kipya watakuwepo. Wasahii kama Ali Kiba, Nandy na wengine wengi watakuwepo” alisema Shekimweri.  

Akiongelea maandalizi ya tukio hilo, alisema kuwa maandalizi yamekamilika. “Kwa niaba ya kamati ya maandalizi ikiongozwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na wizara za kisekta, maandalizi yote yamekamilika. Milango ya uwanja wa Jamhuri itakuwa wazi kuanzia saa 11 alfajiri”

Kuhusu ulinzi na usalama, alisema kuwa vimeimarishwa na kuwaomba wakazi wa Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi sana kumpokea na kumshangilia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiongelea tahadhari ya ugonjwa wa Uviko-19, alisema kuwa tahadhari ya Uviko-19 imezingatiwa. Barakoa zitakuwepo na wananchi watapatiwa Pamoja na vitakasa mikono vitakuwepo.

Sensa ya watu na makazi mwaka 2021 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa”.