Thursday, January 16

MHE. OTHMAN: TUWASHIRIKISHE WATAALAMU KATIKA KUPAMBANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza kuwa ipo haja ya kupokea na kutendea kazi mawazo ya wataalamu ili kuinusuru Nchi kutokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Othman ameeleza hayo leo ofisini kwake Migombani jijini Zanzibar, alipokutana na Ujumbe kutoka Shirika la ‘CityCon Africa’ uliofika kuwasilisha wazo la haja ya visiwa vya Unguja na Pemba, kujilinda kutokana na tishio kubwa la kumezwa na bahari.
Amesema kuwa mawazo ya wataalamu, uzoefu, maarifa na stadi muhimu zinazolenga kuibakisha salama Zanzibar kutokana na athari kubwa zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi zinahitajika, sambamba na miradi itakayozingatia njia mbadala za kujenga uchumi wa Nchi na kukuza kipato, bila ya uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Othman amebainisha mambo yanayochangia athari hizo hapa Visiwani kuwa ni pamoja na kasi ya kutanuka kwa miji, harakati zisizojali maeneo muhimu ya uzalishaji, na pia matumizi mabaya ya ardhi, yasiyoendana na ongezeko kubwa la idadi ya watu.
Akitolea mifano ya nchi zilizofanikiwa kukabiliana na athari za matumizi mabaya ya ardhi ambazo zinazolingana na Zanzibar kijeografia, zikiwemo Malaysia na Singapore, Mheshimiwa Othman amesema, “kiujumla tunaweza kufanikiwa kuyakabili yote hayo na kuendelea kujenga uchumi wetu, pindipo tutaweza kujumuisha kikamilifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali pamoja na jamii kwa upana wake”.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Mazingira Zanzibar, Bw. Sheha Mjaja Juma, akitilia mkazo haja ya kuwepo juhudi za kuiokoa nchi kutokana na balaa la kimazingira amebainisha maeneo yaliyokwisha-athirika ambayo athari zake zinadhoofisha moja kwa moja maendeleo ya uchumi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Ametaja kuwa mfululizo wa tafiti za kitaalamu tangu mwaka 2011, umebainisha changamoto katika sekta za kilimo na uzalishaji, uvuvi na upatikanaji wa mvua hapa visiwani, uliotokana na athari za moja kwa moja za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha Mjaja amebainisha kuwa Serikali kwa makusudi ilidhamiria kuweka misingi muhimu ya kuelekea kukabiliana na mabadiliko hayo, ambayo ni pamoja na sera ya jumla ya tabianchi ya mwaka 2013, iliyofuatiwa na Sheria ya Mazingira ya 2015 kabla ya marekebisho muhimu yaliyofungua milango ya mahitaji ya mbinu ya ufukiaji wa ardhi (land reclamation) ya mwaka 2019.
Akiwasilisha wazo la mapendekezo ya kuisaidia Zanzibar kujiokoa na athari za mabadiliko ya tabianchi, Kiongozi wa Ujumbe huo ambaye ni Mshauri wa Mambo ya Kibenki na Uwekezaji wa Shirika la CityCon Africa, Bw. Simbarashe Manwere, amesifia Sera bora na Sheria makini za hapa visiwani, zinazowezesha kufanikisha azma hiyo.
Manwere aliyeambatana na Mwakilishi Mkaazi wa CityCon Africa, Bw. Augustine George Kiula, amesema siyo siri kwamba visiwa vya Unguja na Pemba vinakabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na athari za kimazingira na uchache wa ardhi, ila lengo la shirika lake ni kutumia uzoefu na mbinu za kitaalamu, walizotumia katika nchi mbali mbali ikiwemo Uholanzi, pamoja na  kupata mashirikiano ya Serikali na jamii kwa ujumla ili kuisaidia Zanzibar kupambana na tatizo hilo.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar