JUMLA ya Vilabu 16 kutoka katika jimbo la Wawi, vinavyoshiriki ligi za madaraja mbali mbali Kisiwani Pemba, vimekabidhiwa fedha taslimu kwa ajili ya kulipia ada ya usajili wa mashindano, katika madaraja wanayoshiriki kutoka kwa Mbunge na Mwakilishi wa jimbo hilo.
Vilabu vilivyokabidhiwa fedha hizo ni daraja la kwanza walipata shilingi laki nne, daraja la Pili Mkoa walipewa laki tatu na nusu na daraja la Pili Wilaya walipatiwa shilingi laki mbili, fedha hizo ikiwa ni ahadi zilizotolewa na mbunge na mwakilishi wa jimbo hilo.
Akizungumza na viongozi wa Vilabu aliyekuwa Mdhamini wa Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba, Fatma Hamad Rajab aliwapongeza viongozi hao wa jimbo la wawi, kwa kuwasaidia fedha za usajili vilabu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi walizozitoa wakati wakiomba kura.
Alisema vilabu vingi vimekuwa vikishindwa kuendelea mbele kutokana na kutokua na kukosa ada ya mashindano, hali inayopelekea soka kushuka chini.
“Ndugu sote tunatambua kama mpira kwa sasa ni gharama, mpira ni ajira mpira ni afya, vizuri tukawa mshati wambele katika masuala haya”alisema.
Hata hivyo aliwataka viongozi wa majimbo kuhakikisha wanabadilika katika utendaji wa kazi, kwa kuibua vipaji vipya vya wanamichezo.
Mwakilishi wa jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, alisema lengo la kukabidhi fedha hizo ni kulipia ada ya mashindano kwa vilabu, ili viweze kushiriki ligi hiyo kwa msimu wa 2020/2021.
Alisema vilabu vingi vilivyomo ndani ya jimbo hilo ni masikini, fedha hizo zitaweza kuwainua na kuweza kushiriki katika ligi kwa msimu huo.
Aidha aliwataka viongozi wa vilabu hivyo kutumia nafasi yao ya michezo kwa kuhakikisha wanaondosha uhasama au chuki au kutengana kwa kisingizio ni siasa na wakati wa siasa umepita.
Mbunge wa jimbo la Wawi Khamis Kassam Ali, alisema bado changamoto ya usafishaji ya uwanja ikiendelea kwani kwa kuazia wataanza na uwanja wa Ndugu kitu unaotumiwa na Timu ya Machomanne United.
Akitoa neon la shukurani Kiongozi wa Timu ya Small Ranger Nassor Seif Said, aliwatak viongozi hao kuhakikisha wanarudisha heshima ya marehemu Dk.Omar Ali Juma, kwa kurudisha mashindano hayo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chake Chake Khamis Salum Khamis, aliwataka viongozi wa vilabu vilivyokabidhiwa fedha za usajili, kuhakikisha wanaziawasilisha katika vilabu vyao na kutumiwa kwa lengo lililokusudiwa.