Kenneth Kaunda – Mwana wa Afrika aliyekuwa na ushawishi ndani na nje ya Zambia
Kenneth Kaunda alikuwa ni mmoja wa viongozi waasisi wa Afrika mpya, wakati nchi yake ilipoondokana na ukoloni na kuwa taifa huru.
Kiongozi huyu ambaye alikuwa na haiba ya uchangamfu, alisifiwa kama kiongozi aliyekuwa na msukumo wa kisasa katika bara licha ya kwamba mwanzoni aliikataa dhana ya demokrasia ya vyama vingi.
Akiwa mwana wa Afrika aliyejitolea, alianza kazi ya kuijenga Zambia mpya, huru kuamua njia yake katika masuala ya kimataifa.
Lakini usimamizi duni wa uchumi ulisambabisha umaarufu wake kushuka, na akaondolewa madarakani baada ya kushindwa kwa kura wakati uchaguzi huru ulipofanyika mwaka 1991.
Kenneth David Kaunda alizaliwa tarehe 28 Aprili 1924 katika kituo cha wamishonari karibu na mpaka baina ya Rhodesia Kaskazini (Zambia ya sasa) na Congo.
...