NA FATMA HAMAD FAKI
Wavuvi wanaotumia bandari ya Shumba mjini Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wamemuomba Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dr Hussein Ali Hassan Mwinyi kutekeleza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni juu ya kuwawekea Boti ya uokozi katika bandari hiyo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huko bandarini kwao shumba mjini wamesema kutekeleza ahadi kutatoa matumaini kwa wananchi katika Nyanja mbali mbali za kimaendeleo.
Aidha wananchi hao wamesema wanamatumaini makubwa ya kupata maendeleo katika Serikali ya awamu ya Nane kwani imeanza kuonesha dalili njema kwa wananchi wake.
Sambamba na hayo wavuvi hao wamesema ingawa hali ya maisha bado ni ngumu lakini wamefurahishwa kwa hali ya utulivu na amani iliyopo huku wakifanya shughuli zao bila ya kubughudhiwa na mtu yoyote.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wavuvi wa bandari hiyo Hussein Rashid amemkumbusha Rais Mwinyi kuifanya bandari ya shumba mjini kuwa huru kwa wasafiri wanaotoka bandari ya Shimoni Kenya na pamoja na kisiwa cha Pemba.
Hata hivyo amewataka wananchi wote kushirikiana kwa pamoja katika harakati za kimaendeleo bila ya kubaguana kutokana na tafauti za kisiasa
Nae Afisa mkuu idara ya maendeleo ya Uvuvi Pemba Sharif Muhammed Khamis amewatoa hofu wavuvi hao na kusema kuwa muda utakaporuhusu watapatiwa wanachokihitajia.