PPC YAADHIMISHA MIAKA 30 YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI KISIWANI PEMBA.

NA ABDI SULEIMAN.

AFISA Mdhamini wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Pemba Hafidh Ali Mohamed, amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao katika kuelimisha jamii juu ya ulipaji wa kodi na matumizi sahihi ya risiti za elektroniki.

Alisema kuwa, waandishi wa habari ndio daraja la mawasiliano hivyo, ni vyema kuitumia taaluma ya uwandishi wa habari katika uwandaaji wa makala na vipindi vya kila siku kwa lengo la kuielimisha jamii.

Mdhamini Hafidhi aliayeleza hayo wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari Pemba, katika mkutano wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari Duniani, maadhimisho yaliyofanyika Mjini Chake Chake na kuandaliwa na chama cha waandishi wa habari Pemba (PPC) kwa Ufadhili wa UTPC na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

Alisema hili ni Jambo adhimu sana kwa sababu nyinyi waandishi wa habari ni daraja la mawasiliano, hivyo elimu watakayoipata itawasaidia kuwajengea uwelewa juu ya masuala ya kodi.

“Uwelewa huu utawasaidia kuelimisha jamii katika uwandishi wa habari na uandaaji wa vipindi vya kila siku, sasa habari zenye ueledi na zilizofanyiwa utafiti wa kutosha zitaandikwa kwa wingi,”alisema.

Aidha alisema, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na dk. Hussein Ali Mwinyi inahimiza sana ulipaji wa kodi kwa kupitia mifumo mipya, ambapo ni jambo muhimu na linahitaji wananchi wengi kujengewa uwelewa.

“Sote tunafahamu umuhimu wa kodi katika kuleta maendeleo ya nchi, juhudi za maendeleo zinazoletwa na serikali zetu mbili haziwezi kufanikiwa bila ya ulipaji wa kodi ambayo inasaidia kugharamia miradi mbali mbali ya maendeleo,”alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari wa Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma, alisema PPC ni miongoni mwa klabu 28 zilizopo Tanzania chini ya mwevuli wa umoja wa vilabu vya habari (UTPC).

Alieleza, PPC katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari, imeamua kuwapatia elimu ya kodi na umuhimu wa matumizi ya risiti za elektroniki waandishi wa habari, ikiwa ni njia moja ya kuhakikisha mapato yanaingia katika sehemu husika.

Alisema PPC ni moja  ya klabu bora Tanzania ambao inatambulika katika umoja huo na wafadhili wao ikiwemo ubalozi wa Sweeden katika shirika lake la Misaada la SIDA.

“Licha ya wanachama wetu kuona labda PPC ni klabu ambayo haina maana yoyote kiutendaji ni dhaifu, niwaeleze kama kuna klabu 10 bora Tanzania, basi niwaeleze klabu ya Pemba Press Club ni miongoni mwa hizo na ndio maana hata UTPC inapopanga mipango ya kiutendaji PPC huwa inashirikishwa kwa namna moja ama nyengine,”alisema.

Akiwasilisha mada Afisa TEHAMA kutoka mamlaka ya mapato Zanzibar ZRA Pemba Khairat Said Soud, alisema changamoto zinazotokana na biashara katika ukusanyaji wa kodi ni wafanyabiashara wengi kutokufanya usajili na kupelekea uvunjaji wa mapato.

“Wafanyabiashara kutokutoa risiti na wananchi kutokua na mwamko wa kudai risiti, kutoa taarifa za mauzo zenye viwango vya chini ni miongoni mwa changamoto ambazo mamlaka inakabiliana nazo wakati wa ukusanyaji wa kodi”, alisema.

Kwa upande wao waandishi wa habari walisema, suala la ulipaji wa kodi linahitaji uzalendo hivyo, ni vyema ZRA ikaandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii ili ipate uwelewa mpana juu ya ulipaji wa kodi na kudai risiti pale wanaponunua bidhaa.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 3 ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ya siku hiyo ni “KUUNDA MUSTAKBALI WA HAKI, UHURU WA KUJIELEZA KAMA KICHOCHEO CHA HAKI NYENGINE ZOTE ZA BINAADAMU”.