PPC yawapatia mafunzo Timu ya wahamasishaji wa amani na utatuzi wa migogoro.

NA MARYAM SALUM, PEMBA

JAMII imetakiwa kuacha tabia ya kuwaazima wanasiasa akili zao,hasa  wakati wa kipindi cha Uchaguzi na wakakubali kuwa chanzo cha kuvunja amani kwani hawawezi kubaki salama.

Hayo yalielezwa na wajumbe wa timu ya wanahamasishaji wa washiriki wa mijadala ya amani na utatuzi wa migogoro kutoka Klabu ya Waandishi wa habari Pemba(PPC), wakati wakichangia mada katika ukumbi wa Samael Gombani.

Walisema kuwa kinapofikia kipindi cha kampeni sambamba na uchaguzi, wapo baadhi ya watu hushawishiwa na wanasiasa katika   uchafuzi wa amani, jambo ambalo linapelekea kuwa na jamii yenye migogoro baadae.

Walisema jamii lazima ikae na kutafakari sambamba na kutumia akili na maarifa yao kutokubali kuwa vyanzo vya uvunjifu wa amani kwa maslahi na kustakabali wa baadae.

“Kutokana na matatizo mengi yanayojitokeza kwa jamii pale amani inapotoweka, ni lazima jamii sasa kukaa kubadilisha mfumo wa maisha walionao , ili watumie akili na maarifa yao binafsi kwa kutokubali kuwa vyanzo vya uvunjifu wa amani na badala yake kupelekea kuwepo kwa migogoro mingi kwenye jamii, kwa maslahi ya watu wachache” walieleza wajumbe hao.

Sheikh Said Abdalla Nassor kutoka taasisi ya Samael Pemba, alisema jamii kwa sasa imeweka mbele siasa kuliko maamrisho ya  Dini na hivyo inapelekea kufanya mambo yasio endana na mila na silka za kibinaadamu.

Aliiomba jamii kuelewa kuwa kila mmoja ni mlinzi wa amani kwa nafasi yake alionayo na kuwa na uthubutu bila woga katika kuhubiri suala la amani na utatuzi wa migogo inayojitokeza katika jamii.

Kwa upande wake Sheikh Said Ahmad Mohammed  msaidizi katibu wa mufti Pemba alieleza ni vyema  wasuluhishi wa migogoro pale inapotokea kuwa na hekima na busara kabla ya kukabiliana na migogoro hiyo.

Aidha alisema kablaya kutaka kuingia kwenye utatuzi wa migogoro wazingatie wakati wa kufanya usuluhisho wa migogoro na waangalie madhara ya migogoro hiyo.

Alisema kunavipindi vya mpito wananchi hususan Vijana hutumiliwa na watu kuvunja amani kwa maslahi yao na wakimaliza kipindi hicho hubakia wakajilaumu  huku wale waliowatumia wakiwa na raha zao.

“ Nawasihi wananchi ifike muda tuwe na kauli thabiti na tukatae kwa kauli moja hatutaki kutumiliwa na nyinyi kwa maslahi yenu tuanataka amani ndani ya nchi yetu,”alieleza.

Nae Mjumbe wa kamati wa uhamasishaji na washiriki wa mijadala kuhusiana na amani na utatuzi wa migogoro Pemba, Said Moh’d Ali aliitaka jamii kuwa tayari kutumia akili zao na kuweka mbele uzalendo wa taifa lao kwa kutokubali kutumiliwa kwa maslahi ya watu wachache na kuvuruga amani na utulivu.

Aliwataka wajumbe wenzake kuhakikisha wanakwenda kuifanya kazi hiyo kwa kuifahamisha jamii iliowazunguka umuhimu wa kuwepo amani ndani ya familia , Jamii na Taifa kwa ujumla katika harakati za kujiletea maendeleo.

Said Moh’d ambae pia ni mwenyekiti mstaafu wa PPC, aliwasihi wajumbe wenzake kukubali kuilinda na kuitetea amani ya nchi ili iweze kudumu sambamba na kuwafahamisha jamii madhara ya kutokuwepo amani ndani ya nchi.

“ Jamii isikubali kuwa ngazi ya kuwapa uweze Viongozi wa kisiasa  kuwarubuni vijana kuhatarisha amani na ifike muda wawakatae bila woga,”alisema.

Alisema wazazi na walezi nao wanwajibu wa kuwalea watoto wao katika mazingira mazuri ya ulinzi wa amani kwani wakiwaacha kuwafanya hivyo watakuwa rahisi kurubuniwa na watu kwa maslahi yao.

Aliitaka jamii kuacha matamanio na kuondowa utu wao kwa kukubali maneno na hata fedha chache kwa kuvuruga amani yao lazima watumie akili pale wanapapandikizwa chuki wafikirie hatma yao na taifa lao.

Alifahamisha ni vyema jamii ikawa na uthubutu wa kweli kwa ulinzi wa amani yao ili Kisiwa cha Pemba na Zanzibar kwa ujumla ibakie na amani yake.

Nae maalim Moh’d Ali kutoka YUNNA alisema bila ya amani hakuna maendeleo yoyote hivyo jamii ianche tabia ya kuona amani inachafuliwa na kusema baadhi ya mambo hayawahusu kwani kila mmoja ni mlinzi wa amani ndani ya taifa lake.

Aliwataka wanajamii kuweka mbele utaifa wao na kwa kuwa tayari kulinda amani na kukubali kusuluhisha migogoro pale inapotokea kwa nguvu zao zote kwa kujiamiani kuwa wao wanahaki ndani ya nchi hii.

Alisema uvunjifu wa amani kwa Zanzibar inavunjwa kwa ukosefu wa imani ya Dini kwani asilimia kubwa ya Wazanzibar wanadini zao na hakuna hata moja inayohimiza wafuasi wake wachafue amani ispokuwa inawataka waendeleze amani kwa kumuheshimu kila mtu.

Hata hivyo aliwataka Viongozi wa kisiasa wajiaminishe kwa jamii wasiwe wasaliti wakati wa mpito kama kipindi cha uchaguzi kwa kuharibu amani iliopo kwa kuwarubuni wananchi hususan vijana kufanya hivyo.

“Naiomba jamii muwe na ridhaa, katika kuzuwia , kudhibiti amani yetu hao wanaokuja kuwashawishi kuvunja amani muwakatae,”alisema.

Aidha mjumbe wa kamati hiyo Dkt , Amour Rashid Ali Mkaguzi mkuu wa Elimu mkoa wa Kusini Pemba, aliwataka wajumbe wenzake kuhakikisha pale watapokwenda kwa jamii kusuluhisha migogoro wasiwe mahakimu bali wawe wasuluhishaji kwa kutafuta vyanzo vya migogoro.

Alisema lazima wawe na weledi wa kutosha kwa kufanya utafiti na kumsikiliza kila mmoja kati ya wale wenye migogoro na kutumia lugha mzuri inayoeleweka na kukubalika ili iwe rahisi kwao.

Nae Rukia Ibrahim Kombo kutoka sauti ya vijana pemba alisema kila mmoja anauwezo wa kutatuwa migogoro pale inapotokea hivyo kila mmoja awe mkweli kuhusu hilo .

Aliwataka wajumbe wenzake kuchukuwa hatuwa za haraka na kukataa kata kata kutumiliwa pale wanapoona mambo hayaendi sawa na kutokuwa woga katika kutekeleza majukumu yao.

“ Ni vyema sisi ambao tumepewa jukumu hilo tujitayarishe kabla ya kuenda kwenye migogoro pale inapotokea ili iwe rahisi kuipatia suluhisho,”alisema.

Kwa upane wake Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC) aliwataka wajumbe hao kuelewa kuwa wao ndio wenye dhima ya kuilinda , kuishawishi jamii katika ulinzi wa amani na wasiwe na kinyume katika kuifanikisha kazi hiyo kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekitiwa  Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi ameazimia kuifanya Pemba kuwa eneo la uwekezaji na utalii hivyo bila ya kuwepo amani hilo haliwezi kufikiwa ni lazima kila mmoja ahubiri amani pale anapopata fursa ya kuzungumza na jamii.

“ Tumewachaguwa nyinyi viongozi wa dini, taasisi zisizo za Serikali na baadhi ya waandishi wa habari kwa umuhimu wenu katika jamii hivyo muelewe kuwa Pemba na Zanzibar kwa ujumla inawaangalia nyinyi,”alisema Bakar.

Aliwataka kufanya kazi zao kwa weledi bila ya kuweka mbele maslahi ya mtu mmoja mmoja kwa kutowa kile walichojaaliwa na Mwenyeezi Mungu katika kuishawishi jamii na wafuasi wao kuhusiana na mambo mbali mbali ikiwemo amani .

Kamati hiyo ya ushawishi na ushiriki wa mijadala inayohusiana na amani na utatuzi wa migogoro imeundwa na klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC) kupitia mradi wake wa SAUTI YANGU, AMANI YANGU, HATIMA YANGU unaotekelezwa kwa mashirikiano ya shirika la Search for Common Ground na Foundation for Civil Society kwa ufadhili  wa umoja wan chi za  Ulaya (EU) kwa lengo la kudumisha amani na utatuzi wa migogoro kisiwani Pemba na Zanzibar kwa ujumla.