NA KHADIJA KOMBO-PEMBA.
Waandishi wa habari Kisiwani Pemba wametakiwa kuwa makini kwenye kutumia kalamu na sauti zao katika kuhubiri amani, kwani wao wanauwezo mkubwa wa kuwahamasisha wananchi juu ya kuiendeleza amani iliyopo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumiya ya waandishi wa Habari Kisiwani Pemba PPC Bakar Mussa Juma wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari wa vyombo tofauti walioko Kisiwani Pemba juu ya umuhimu wa kuepuka migogoro na kujenga amani nchini.
Amesema Waandishi wahabari ni kiungo muhimu katika ujenzi wa amani ndani ya jamii iwapo watafuata Maadili na kanuni za kazi zao.
Akiwaswilisha mada juu ya umuhimu wa amani na dhima ya vyombo vya habari katika kujenga amani Mwenyekiti mstaafu wa Pemba Press Club Said Mohammed Ali amesema waandishi wanapaswa kutumia taaluma yao katika kuihamasisha jamii juu ya kuepuka migogoro na mifarakano kwani ndio chanzo kikuu cha uvunjifu wa amani.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wamewaomba wahariri kuwa makini katika kuziangalia habari hasa katika matumizi ya lugha ili isije ikawa chanzo cha kuleta machafuko ndan iya jamii.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanayoendeshwa na Jumuiya hiyo ni kufuatia mradi wa Sauti Yangu Amani yangu Hatima yangu kupitia Mradi mkuu wa jenga amani yetu unaosimamiwa na Foundation for civil society kwa kushirikiana na Search for Common Ground kwa hisani ya European union